Zaidi ya Wakenya 800,000 walipokea Hustler Fund bila ya kujisajili

Gathungu alibaini kuwa wakopaji ambao hawakusajiliwa walipokea fedha ndani ya miezi saba ya kwanza.

Muhtasari

• Bi Gathungu amefichua serikali iliwapa wakopaji milioni 464.7 bila ya kusajiliwa kwenye Hustler Fund.

•Haikuwezekana kuthibitisha kama malipo ya mikopo yaliyotolewa kwa wateja mbalimbali yalifuata kanuni na iwapo mikopo hiyo ilikuwa sahihi

Mkaguzi Mkuu Nancy Gathungu
Image: MAKTABA

Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali Nancy Gathungu amefichua kwamba serikali iliwapa wakopaji milioni 464.7 bila ya kusajiliwa kwenye Hustler Fund.

 Gathungu alisema kuwa fedha za umma zingeweza kuwa zilipotea kupitia Hustler Fund. Gathungu alifichua kuwa zaidi ya wakenya 800,000 walipokea mikopo kutoka kwa kituo hicho licha ya kutojisajili.

Vilevile, mkaguzi huyo alibaini kuwa wakopaji ambao hawakusajiliwa walipokea fedha ndani ya miezi saba ya kwanza ya uendeshaji wa Hustler Fund.

“Ilibainika kuwa watu 808,047 walipewa malipo ya awali ya mkopo wa shilingi 464,700,721 kabla ya kuchagua huduma ya kifedha," Gathungu alisema katika ripoti yake kuhusu fedha za serikali ya kitaifa kwa mwaka wa kifedha wa 2022/2023.

"Katika mazingira hayo, haikuwezekana kuthibitisha kama malipo ya mikopo yaliyotolewa kwa wateja mbalimbali yalifuata kanuni na iwapo mikopo hiyo ilikuwa sahihi na haina dosari," aliongeza.

Hazina ya Hustler Fund ya shilingi bilioni 50 ilizinduliwa na Rais William Ruto mnamo, Novemba 30, 2022. Ruto alisema hazina hiyo inatoa fursa kwa zaidi ya wakenya milioni nane ambao hawakuorodheshwa katika Taasisi ya Kurejelea Mikopo (CRB).

Wakenya hufikia huduma hiyo kupitia msimbo wa USSD (*254#). Kiwango cha juu cha mkopo kinatolewa kulingana na uwezo wa mkopaji kurejesha au alama ya mkopo.

Benki za biashara zinateseka huku wakenya wakikosa kulipa mikopo kwa maslahi yanayoongezeka, ripoti ya CBK Hustler Fund iliongezeka mwaka mmoja baada ya bidhaa hiyo kuzinduliwa.

Ruto aliweka kikomo cha mkopo kulingana na alama za ulipaji mikopo za wakopaji. Rais alitangaza kwamba wakopaji walio na mikopo 10 waliona ongezeko la kikomo cha 100%, wakati wale walio na mikopo zaidi ya mitano walipata nyongeza ya 50% ya kikomo chao cha mkopo.

Alifafanua kuwa siku za nyuma, wakopaji hawakuwa na njia mbadala na waliona kulazimika kutafuta mikopo kutoka kwa majukwaa mbadala ambayo yaliweka viwango vya juu vya riba.

Kiwango cha riba cha Hustler Fund ni 8% kwa mwaka, na zaidi ya shilingi bilioni 32  zimepeanwa. Muda wa kurejesha mkopo umepangwa ndani ya siku 14 baada ya malipo. Hazina ya Kitaifa ilichapisha kanuni za kuzingatiwa ikiwa mtu anataka kufaidika na bidhaa hiyo.