Ruto amwagiza Gachagua kuwa mpatanishi katika mzozo wa uchaguzi wa UDA Nairobi

Kura hizo za kaunti ya Nairobi zilihusisha pande mbili zinazomuunga mkono Gavana Johnson Sakaja na Mbunge wa Embakasi Kaskazini James Gakuya.

Muhtasari

• Kura hizo za kaunti ya Nairobi zilihusisha pande mbili zinazomuunga mkono Gavana Johnson Sakaja na Mbunge wa Embakasi Kaskazini James Gakuya.

• Katika kutafuta suluhu, Ruto alimtaka naibu wake kuongoza mazungumzo kati ya kambi hizo mbili na kutafuta mwafaka.

Image: DPCS

Rais William Ruto amemuagiza Naibu wake Rigathi Gachagua kuongoza mazungumzo ya kisiasa ili kuibua mzozo wa uchaguzi wa UDA kaunti ya Nairobi.

Kura hizo za kaunti ya Nairobi zilihusisha pande mbili zinazomuunga mkono Gavana Johnson Sakaja na Mbunge wa Embakasi Kaskazini James Gakuya.

Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi ya UDA mnamo Jumamosi ilifutilia mbali uchaguzi wa Kaunti ya Nairobi ambao ulipangwa kufanywa Jumatatu kufuatia mzozo.

Mahakama ya Mizozo ya Vyama vya Siasa ilisitisha uchaguzi mnamo Juni 6 kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa na moja ya mirengo hadi kesi hiyo iamuliwe.

Katika kutafuta suluhu, Ruto alimtaka naibu wake kuongoza mazungumzo kati ya kambi hizo mbili na kutafuta mwafaka.

“Huko Nairobi ambako kambi mbili zinazozana kuhusu mchakato wa uchaguzi, Ruto aliagiza Naibu Rais aongoze katika mazungumzo yatakayoleta suluhu la kisiasa,” taarifa ya chama cha UDA ilisema.

Rais alitoa uamuzi huo Jumamosi jioni baada ya kuongoza kikao cha Halmashauri Kuu ya UDA kilichofanyika Ikulu baada ya siku nyingi za vuta nikuvute.

Chama hicho kilisema uamuzi ulifanywa kwamba uchaguzi wa Nairobi ufanyike katika siku zijazo ili kuwawezesha wajumbe wa chama kuchagua viongozi wao.

"Kura za maoni za Nairobi zinaweza kufanywa siku moja na kaunti zingine mbili," alisema.

Gachagua, mkuu wa pili nchini anasemekana kuunga mkono mrengo wa Gakuya ingawa mbunge huyo amekanusha ripoti hizo.

Haijabainika jinsi DP atakavyoendesha mazungumzo hayo ikizingatiwa kwamba amehusishwa na kambi ya Gakuya.

Mrengo wa Gakuya unaripotiwa kutaka uchaguzi ufanyike kwa kutumia mfumo wa mwongozo huku kambi ya Sakaja ikitaka mchakato safi wa kidijitali kuwachagua maafisa wa kaunti.

Kufuatia uchaguzi wa Jimbo hilo uliofanyika kote Nairobi, kambi ya Sakaja ilipata ushindi, na kupata kura 240 dhidi ya kura 340 za Gakuya.