St.Johns Ambulance yakanusha kusafirisha wabunge wakati wa maandamano

Uvumi ulienea kwenye mitandao ya kijamii kuwa magari ya kubebea wagonjwa yaliyoingia katika eneo la bunge yalikuwa yakiwahamisha wabunge waliokwama

Muhtasari

•Shirika la St. Johns Ambulance lilidai kuwa uvumi kama huo waweza kufanya wafanyikazi wao kuvamiwa na umma ambao ulikuwa unapinga mswada wa fedha.

• Shirika hilo lilisema liliwahamisha jumla ya watu 17 ambao walijeruhiwa wakati wa maandamano hayo mabaya.

Image: st.John Ambulance

St John Ambulance imekanusha madai ya mitandao ya kijamii kwamba ambulensi zake zilitumika kuwahamisha wabunge waliozingirwa baada ya waandamanaji kuvuka usalama na kuvamia majengo ya bunge.

Katika taarifa ya Jumatano, mtoa huduma ya matibabu ya dharura alisema uwepo wa ambulensi yake katika Bunge Tower ilikuwa sehemu ya jukumu lake la kukabiliana na dharura wakati wa shida.

"Kama shirika la kushughulikia dharura, tunalazimika kujibu simu zote za dharura bila upendeleo. Ambulensi yetu iliitwa kujibu kisa kimoja cha majeruhi katika Bunge Tower pamoja na matukio mengine kadhaa yaliyojibiwa wakati wa maandamano kote jijini,” shirika hilo lilisema.

St John ilisema iliwahamisha jumla ya watu 17 ambao walijeruhiwa wakati wa maandamano hayo mabaya. Ilisema wawili waliokuwa katika hali mahututi walikimbizwa katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta huku waliosalia wakipelekwa katika hospitali za Nairobi West na Mbagathi.

Uvumi ulienea kwenye mitandao ya kijamii kuwa magari ya kubebea wagonjwa yaliyoingia katika eneo la bunge yalikuwa yakiwahamisha wabunge waliokwama. Shirika hilo, ambalo pia lilishutumiwa kwa kuwahamisha wabunge, lilitoa taarifa kukanusha madai hayo na kuonya kwamba uvumi kama huo ni hatari kwa wafanyikazi wake ambao wanaweza kulengwa kwa mashambulizi na umma ulioghadhabishwa na hatua ya wabunge kupitisha Mswada wa Fedha, 2024.

"Magari yetu yameshambuliwa. Wafanyikazi na watu waliojitolea walijeruhiwa. Hatuna mawasiliano au jukumu la kuwasafirisha watu zaidi ya waliojeruhiwa. Uvumi lazima ukome," Shirika la msalaba mwekundu lilisema.

St John Ambulance ilisisitiza wasiwasi huo huo na kuwashauri umma dhidi ya uvumi huo.

"Tunawaomba wananchi kuzingatia usalama wa watoa huduma za dharura na kutoa nafasi kwa magari ya kubebea wagonjwa ili kuwafikia majeruhi na kuwahi hospitali kwa wakati."