Gachagua awataka walimu wakuu kuwa na subira kuhusu pesa za elimu

Gachagua alikuwa akiongea wakati wa kongamano la 47 la kila mwaka la chama cha wakuu wa shule za sekondari kule Mombasa.

Muhtasari

•Naibu rais amewaomba walimu wakuu kuwa watulivu serikali inaposhughulikia pesa za masomo katika shule za sekondari.

•Gachagua aidha aliwaomba walimu kusaidia kudhibiti utumizi wa pombe na madawa ya kulevya miongoni mwa wanafunzi.

DP Gachagua
DP Gachagua
Image: HISANI

Naibu rais Rigathi Gachagua ametoa wito kwa wakuu wa shule za sekondari kuwa na subira na serikali kuhusu kutolewa kwa fedha za masomo.

Wakati wa  kongamano la 47 la kila mwaka la chama cha wakuu wa shule za sekondari nchini Kenya katika shule ya Sheikh Zayed, Mombasa, naibu Rais alikariri kujitolea kwa serikali kwa sekta ya elimu inayostawi.

" Tumekuwa na changamoto za ufinyu wa nafasi ya fedha, na kuongeza deni la umma dhidi ya kupungua kwa mapato. Hatuna duka popote ambapo tunaweza kupata pesa. Tunapokea pesa kutoka kwa walipa kodi. Wakati kuna ucheleweshaji wa kupokea kuna kuchelewa kwa utoaji. Tunajaribu kadiri tuwezavyo kutoa pesa kwa wakati..." Gachagua alisema

Kulingana na Gachagua,serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa kwenye vyuo vya kifundi ili kuwapa vijana ujuzi utakaowafanya wawe na ushindani katika soko la ajira. Hii ni pamoja na ujumuishaji wa utambuzi wa mafunzo ya awali ili kuongeza matarajio kwa watu ambao tayari wana ujuzi unaohitajika lakini hawana hati za kuthibitisha.

“Tumeendelea kuwekeza kwenye TVET kwa sababu ya uwezo wao wa kuzalisha ajira hasa katika Sekta isiyo rasmi ya uchumi wetu ambayo inaajiri zaidi ya asilimia 83 ya wafanyakazi wetu. Katika kutafuta fursa zaidi nje ya mipaka yetu, ujuzi wa hali ya juu ndio pasipoti. Kwa hiyo, lazima kuwe na mabadiliko ya haraka kutoka shule za sekondari hadi vyuo vya elimu ya juu."

Vile vile aliongeza kuwa ; "Pia tumejumuisha utambuzi wa mafunzo ya awali chini ya TVET kama mkakati wa kuongeza matarajio ya ajira kwa watu ambao tayari wana ujuzi unaohitajika lakini hawana hati za kuthibitisha," Naibu Rais alisema.

Aidha Gachagua aliwaomba walimu kusaidia kudhibiti unywaji wa pombe na utumizi wa madawa za kulevya mingoni mwa vijana.

“Mko na sauti sana. Mtusaidie na hii vita ya pombe haramu. Ikibidi unywe, kunywa kitu sahihi ili wale wanaotaka kukuiga waweze kuiga jambo sahihi. Tunza wasichana wetu ili wasiingizwe na watu wabaya. Tunawategemea kama viongozi..." Gachagua alisema.