Martin Luther King III atuma ujumbe wa amani kwa Wakenya

"Baba yangu alisema kutofanya vurugu ni silaha yenye nguvu na ya haki ambayo inakata bila kujeruhiwa na kumwezesha anayetaka," aliongeza.

Muhtasari

•King III, akiwa na mkewe Andrea Waters King aliwataka Wakenya kuepuka kutumia vurugu wakati wa maandamano.

•Zaidi ya hayo, wanandoa hao walitoa wito kwa maafisa wa polisi pia kutumia njia zisizo za vurugu wanaposhughulika na waandamanaji ambao wanatumia haki zao za kikatiba.

Martin Luther King III na Mkewe
Image: Hisani

Martin Luther King III, mtoto wa marehemu mwanaharakati wa haki za binadamu wa Marekani Martin Luther Jr amewashauri vijana wa Kenya kuhusu maandamano yaliyoshuhudiwa nchini.

King, akiwa na mkewe Andrea Waters King aliwataka Wakenya kuepuka kutumia vurugu wakati wa maandamano.

Wanandoa hao waliongeza kuwa maandamano yasiyo ya vurugu ni ishara ya ujasiri wa kimaadili.

Kulingana na King, babake alipendekeza maandamano yasiyo na vurugu ili kuepusha kupoteza maisha na uharibifu wa mali kama ilivyoshuhudiwa siku ya Jumanne katika maeneo mbalimbali ya nchi.

"Baba yangu alisema kutofanya vurugu ni silaha yenye nguvu na ya haki ambayo inakata bila kujeruhiwa na kumwezesha anayetaka," aliongeza.

King alisisitiza kwamba babake alifaulu katika ushindi wake mwingi kwa kuzingatia kabisa njia zisizo za jeuri kushughulikia maswala mengi.

Zaidi ya hayo, wanandoa hao walitoa wito kwa maafisa wa polisi pia kutumia njia zisizo za vurugu wanaposhughulika na waandamanaji ambao wanatumia haki zao za kikatiba.

Andrea aliongeza kuwa Martin Luther King Jr alipendelea njia zisizo za vurugu wakati wa maandamano kwa kuwa zilikubali maoni ya kila mtu.

Aliwataka Wakenya kuzingatia ushauri huu kwani utakuwa ushahidi wa nidhamu na utu wao.

King ambaye pia ni mwanaharakati wa haki za binadamu, alikariri kuwa ulimwengu unawatazama Wakenya wakiendelea kufanya maandamano ya nchi nzima.

"Wakenya na vikosi vya usalama ulimwengu vitazama, onyesheni sauti zenu, inukeni si kwa hasira bali kwa mwito mzuri wa haki.

Baba yangu alisema katika msingi wa kutotumia nguvu kunasimama kanuni ya upendo," alisema.

Wanandoa hao ni miongoni mwa watu wa kimataifa waliotoa wito wa kufanyika maandamano ya amani nchini humo ili kuepusha umwagaji damu na uharibifu wa mali ya umma na binafsi.