Bei ya petroli yashuka kwa Sh1, dizeli Sh1.50 - EPRA

Mamlaka hiyo ilisema kuwa bei ya petroli itashuka kwa Sh1, dizeli kwa Sh1.50 na mafuta taa Sh1.30.

Muhtasari

•Mamlaka ya udhibiti wa nishati na petroli ilisema kuwa  bei ya petroli itashuka kwa Sh1, dizeli Sh1.50 na mafuta taa kwa Sh1.30.

•Hii inaanza kuzingatiwa hii leo Julai 15 hadi Agosti 14 2024.

Image: BBC

Mamlaka ya udhibiti wa nishati na petroli (EPRA) imetangaza kushuka kwa bei ya mafuta katika ukaguzi wa hivi majuzi unaoanza kutumika  hivi leo, Julai 15 hadi Agosti 14.

Katika taarifa iliyotolewa Jumapili 14,Julai 2024 mamlaka hiyo ilisema kuwa  bei ya petroli itashuka kwa Sh1, dizeli kwa Sh1.50 na mafuta taa Sh1.30.

“Bei hizo ni pamoja na kodi ya ongezeko la thamani ya 16% (VAT) kwa mujibu wa masharti ya sheria ya fedha ya 2023, sheria ya kodi (Marekebisho) ya Sheria ya 2020 na viwango vilivyorekebishwa vya ushuru wa bidhaa vilivyorekebishwa kwa mfumuko wa bei kwa mujibu wa notisi ya kisheria Na. 194 ya  mwaka 2020," EPRA ilisema katika taarifa.

Kushuka kwa bei hizo kulichangiwa na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupungua kwa wastani wa gharama ya kutua kwa 'Super Petrol' iliyoagizwa nje ya nchi kwa asilimia 4.65 kutoka dola za Marekani 750.95 ,hadi Dola 716.03 kwa kila mita ya ujazo Juni 2024;

Dizeli ilipungua kwa asilimia 1.19 kutoka Dola za Marekani 690.99 kwa mita ya ujazo hadi Dola za Marekani 682.73  huku mafuta  taa yakiongezeka kwa asilimia 2.01 kutoka dola za Marekani 679.14  hadi Dola 692.80.

Kushuka kwa bei hiyo sasa kunamaanisha kwamba watumiaji jijini Nairobi watalipa Sh188.84 kwa lita moja ya petroli , Sh171.60 kwa lita ya dizeli na Sh161.75 kwa lita moja ya mafuta taa.