Binti ya Macharia Gaitho azungumzia kutekwa kwa babake

Anita alichapisha video mtandaoni ikionyesha baba yake akilazimishwa kuingia ndani ya gari aina ya Probox.

Muhtasari

•"Baba yangu amesafirishwa kwenye kituo cha polisi cha Karen na gari lililomteka. Yupo salama ingawa walitumia nguvu kupindukia," aliandika.

•"DCI hapa wamethibitisha kuwa watekaji walikuwa kweli ni kutoka DCI. Wanadai ni kesi ya kutambuliwa kimakosa." Aliandika Anita.

alikamatwa Jumatano asubuhi
Mwanahabari mkongwa Macharia Gaitho alikamatwa Jumatano asubuhi
Image: HISANI

Anita Gaitho,binti ya mwandishi mahiri Macharia Gaitho, amezungumzia kwenye jukwaa lake la Twitter kuhusu tukio la kutamausha la kutekwa nyara kwa baba yake.

"Baba yangu amesafirishwa kwenye kituo cha polisi cha Karen na gari lililomteka. Yupo salama ingawa walitumia nguvu kupindukia," aliandika.

Anita alichapisha video mtandaoni ikionyesha baba yake akilazimishwa kuingia ndani ya gari aina ya Probox.

Aliongeza, "Tunapiga ripoti ya utekaji sasa."

Pia alibainisha, "Hili ndilo gari lililomteka. Angalieni dereva huyo anayetaka kutugonga tunapokwenda."

Probox hiyo, ilitambuliwa kuwa yenye nambari ya usajili KBC 725J na ilikuwa nyeupe.

"Hawa watu wanasema ni DCI. Walikuwa na bunduki na pingu lakini walikataa kujitambulisha," aliendelea.

"DCI hapa wamethibitisha kuwa watekaji walikuwa kweli ni kutoka DCI. Wanadai ni kesi ya kutambuliwa kimakosa.

Wanatufanya iwe vigumu kuandika ripoti, wanatuambia tuende makao makuu ya DCI. Wanataka tujiandikishe kwao wenyewe?"

Anita, vilevile,  alikuwa na ndugu yake mdogo wakati wa tukio hilo. Taarifa zake ziliwafikia wananchi, ambao walimtia moyo awe imara.

Pia alishiriki picha za nakala ya gazeti iliyoandikwa na baba yake iliyokuwa na kichwa cha habari, "Mapinduzi ya Wananchi Yanakuja."

DCI tangu wakati huo imeeleza kwamba kukamatwa kwa Gaitho ilikuwa kesi ya kutambuliwa kimakosa. Gaitho alikamatwa Jumatano asubuhi katika Kituo cha Polisi cha Karen.