Ujerumani kuchangia dozi 100,000 za chanjo ya mpox kudhibiti mlipuko barani Afrika

Shirika la Afya Duniani limetangaza mpox kuwa dharura ya afya ya umma duniani.

Muhtasari

•Serikali italipatia Shirika la Afya Duniani rasilimali za kifedha kupitia vyombo mbalimbali vya kupambana na mpox.

•Serikali ilikuwa inaangalia njia ya haraka zaidi ya kupata chanjo hizo kwa nchi zilizoathirika, hasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Image: BBC

Ujerumani itatoa dozi 100,000 za chanjo ya mpox kutoka kwa hisa zake za kijeshi kusaidia kudhibiti mlipuko katika bara la Afrika katika kipindi cha muda mfupi na pia kutoa msaada kwa nchi zilizoathiriwa, msemaji wa serikali alisema Jumatatu, Reuters imeripoti.

Serikali italipatia Shirika la Afya Duniani rasilimali za kifedha kupitia vyombo mbalimbali vya kupambana na mpox na pia kusaidia washirika wake barani Afrika kupitia muungano wa chanjo ya GAVI, aliongeza msemaji huyo.

Ujerumani ina dozi takribani 117,000 za Jynneos, ambazo zinahifadhiwa na jeshi la Ujerumani baada ya Berlin kuinunua mnamo 2022.

Shirika la Afya Duniani limetangaza mpox kuwa dharura ya afya ya umma duniani baada ya mlipuko katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kuenea katika nchi jirani na aina mpya ya virusi, clade Ib, ilisababisha wasiwasi kuhusu kasi ya maambukizi.

Serikali ilikuwa inaangalia njia ya haraka zaidi ya kupata chanjo hizo kwa nchi zilizoathirika, hasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, lakini pia Burundi na nchi jirani za Afrika Mashariki, kulingana na msemaji wa wizara ya mambo ya nje.