Mwanariadha Rebecca Cheptegei kufanyiwa mazishi ya kijeshi

Familia imedhibitisha kuwa marehemu alikuwa mwanajeshi wa Jeshi la ulinzi la watu wa Uganda

Muhtasari

•Mzee Cheptegei imedhibitisha kuwa marehemu alikuwa mwanajeshi katika jeshi la la ulinzi la watu wa Uganda hivyo atazikwa kwa heshima za kijeshi.

•Mzee Cheptegei amesema familia inashirikiana na serikali ya Kenya na Uganda kuhakikisha marehemu anazikwa vyema nyumbani kwao Bukwo, mashariki mwa Uganda.

MAREHEMU REBECCA CHEPTEGEI
Image: HISANI

Mwanariadha Rebecca Cheptegei atazikwa kwa heshima za jeshi  nyumbani kwao Bukwo nchini Uganda siku ya Jumamosi  tarehe kumi na nne mwezi huu.

Familia yake ikiongozwa na Mzee Joseph Cheptegei imedhibitisha kuwa marehemu alikuwa mwanajeshi wa Jeshi la ulinzi la watu wa Uganda  hivyo basi atazikwa kwa heshima zote za kijeshi.

Mzee Cheptegei amesema familia inashirikiana na serikali za Kenya na Uganda kuhakikisha marehemu anazikwa kwa heshima nyumbani kwao Bukwo, mashariki mwa Uganda.

Wiki jana, Cheptegei alidaiwa kuvamiwa na mpenzi wake wa zamani ambaye alimwagilia mafuta ya petroli na kumchoma kwa moto kisa kilichopelekea kifo cha Cheptegei katika hospitali ya rufaa na mafunzo ya Moi jijini Eldoret Alhamisi iliyopita.

“Tumeanza matayarisho ya mazishi kumpa mtoto wangu pumziko zuri yatakayofanywa na jeshi  nchini Uganda,” alisema mzee Cheptegei.

Uchunguzi wa maiti kwa mwili wa Cheptegei utafanywa katika hospitali hiyo siku ya Jumatano.

“Usimamizi wa hospitali ulituuliza kufanya uchunguzi wa maiti na tulikubali kwa sababu itatusaidia kujua chanzo haswa kilichomuua na pia itatupa fursa ya kukubali kifo chake tunapoendelea na maombolezi,” alisema mzee Cheptegei.

Baada ya upasuaji wa maiti, mwili utaondolewa katika makafani siku ya Alhamisi asubuhi na kukabidhiwa familia pamoja na jeshi la Uganda na baadaye kupelekwa nyumbani kwake eneo la Endebes kaunti ya Trans Nzoia ambapo utakesha usiku huo.

“Aliishi huko na tutatoa fursa kwa wakaaji wa huko kutoa heshima zao za mwisho pamoja na maombi,” alisema.

Viongozi wa kitaifa kutoka mataifa hayo mawili wanatarajiwa kuhudhuria mazishi.