Mzazi wa mwanafunzi wa Hillside azungumza huku akisubiri taarifa kuhusu mwanawe asiyejulikana aliko

Mzazi Simon Njogu amezidi kutamauka baada ya mwanawe wa gredi ya 7 kutojulikana aliko kwa masaa 72.

Muhtasari

•Simon Njogu mzazi katika shule ya Hillside Academy amezidi kutamauka baada ya kumtafuta mwanawe Kelvin bila ufanisi kwa kipindi cha masaa 72.

•Njogu alidokeza kwa huzuni kuwa itakuwa pigo endapo atampoteza mwanawe ambaye ndiye kifungua mimba katika familia yake.

Picha ya nyumba inayowaka moto
Image: MAKTABA

Simon Njogu ambaye ni mzazi wa mwanafunzi kutoka shule ya hillside iliyoko katika kaunti ya Nyeri, ameshikwa na huzuni baada ya kumtafuta mwanawe kwa muda wa masaa 72, bila kumwona kufuatia moto uliozuka katika shule hiyo na kusababisha takriban wanafunzi 21 kupoteza maisha yao na kuwaacha wengine na majeraha.

Ni kisa ambacho kwa sasa kimezua hali ya huzuni hususan kwa wazazi na kwa taifa kwa ujumla. Njogu anasimulia vile alivyopokea taarifa za mkasa huo.

Katika mahojiano na Citizen TV, Njogu alielezea jinsi alivyosikitika kwa kupotea kwa mtoto wake kwa jina la  Kelvin, huku akisema ni mwanawe wa kwanza kwenye familia na yuko na matarajio makubwa kwake ili amsaidie maishani.

Njogu, alisema kuwa kufikia sasa hajaweza kupokea taarifa zozote kuhusiana na mwanawe. Aidha,mzazi huyo alikiri kuwa yuko tayari kwa taarifa zozote kuhusu mwanawe.

Alibainisha kwa huzuni kuwa watu wamekuwa wakimtembelea ili kumpa pole kwa mtoto wake,licha ya kuwa bado hajapatikana.

"Kufikia sasa hatujui mahali aliko,watu wamekuwa wakinitembelea nyumbani kwangu kunipa pole,tuko na masahibu mengi endapo tutampoteza mtoto wetu hasa mimi,kwasababu ndiye kifungua mimba".

Njogu alielezea vile amekuwa akijinyima ili mwanawe apate masomo hasa akijinyima mlo ili kupata karo ya mwanawe Kelvin.

Kwa sasa ni kitendawili ambacho hakijaweza kuteguliwa huku maswali ambayo hayana majibu yakizidi kuibuka kila kuchao kwa familia husika.

'Kile chumba cha kulala mbona hakukua na mlinzi wala matroni,tungejua nani alizembea katika kazi yake,ni maswali ambayo tunazidi kujiuliza kama wazazi.Kama wazazi tumefanya wajibu wetu wa kulipa karo na sasa tunataka taarifa kamili kutoka kwa shule'. Njogu alieleza.