EACC yamkamata mwenyekiti wa Muungano wa Mashirika ya Kiraia

Anashukiwa kudai hongo ili kuwacha kufuatilia madai ya ununuzi katika shirika moja la serikali

Muhtasari

• Mwenyekiti wa muungano wa vyama vya kiraia aliachiliwa kwa dhamana ya polisi wa madai ya ufisadi.

• Agoro anadaiwa kumtapeli afisa mkuu mtendaji wa shirika la serikali shilingi milioni 3.

Makao yatume ya maadlili na kupambana na ufisadi
EACC Makao yatume ya maadlili na kupambana na ufisadi
Image: MAKTABA

Jumatano, Mwenyekiti wa Muungano wa Mashirika ya Kiraia ya Kenya Peter Odhiambo Agoro aliachiliwa kwa dhamana ya polisi baada ya kukesha korokoroni.

Agoro alikamatwa Jumanne katika hoteli moja jijini Nairobi na maafisa wa tume ya maadili na kupambana na ufisadi EACC na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Kilimani.

Mshukiwa alikamatwa kwa madai ya kumtapeli afisa mkuu mtendaji wa shirika moja la serikali shilingi milioni tatu.

Taarifa ya EACC imesema kuwa hela hizo zilikuwa za kumshawishi asiendelee kufuatilia madai dhidi ya afisa mkuu mtendaji wa shirika husika kuhusu madai ya makosa katika manunuzi.

EACC imezidi kusema kuwa mshukiwa alikubali ombi la mlalamishi kupunguza hela hadi shilingi milioni 2 ambazo zingelipwa katika awamu mbili.

Awamu ya kwanza ilikuwa malipo ya shilingi milioni 1.5 kisha kumaliziwa kwa shilingi laki tano.

Agoro alikamatwa katika operesheni iliyofanywa na EACC muda mchache baada ya kupokea malipo ya kwanza ya shilingi milioni 1.5 kwa sarafu ya dola.