Chuo kikuu cha Moi chakabiliwa na uhaba wa kondomu

Afisa wa afya ya umma ametahadharisha wanafunzi dhidi ya kufanya mapenzi kiholela

Muhtasari

• Wanafunzi wameshauriwa kuwa waaminifu katika mahusiano yao au kununua bidhaa hiyo muhimu madukani.

Kenya yakabiliwa na uhaba wa kondomu
Kenya yakabiliwa na uhaba wa kondomu
Image: BBC

Chuo kikuu cha Moi jijini Eldoret kimewaonya wanafunzi wake kuwa kuna uhaba wa mipira ya kondomu katika chuo hicho.

Kupitia taarifa kwa wanafunzi kutoka kwa idara ya chuo cha sayansi ya afya chuo hicho kimeelezea kuwa kinakumbwa na uhaba mkubwa wa kondomu.

Taarifa hiyo ilitiwa sahihi na afisa wa afya ya umma P.I Sekenkei mnamo tarehe 19, Septemba  iliwaonya wanafunzi na wafanyakazi wa chuo hicho.

Onyo hilo linajiri siku chache baada ya kusajili wanafunzi wapya ambao wamejiunga  na chuo hicho.

Memo iliyotolewa katika chuo cha Moi tarehe 19 Septemba
Memo iliyotolewa katika chuo cha Moi tarehe 19 Septemba

"Tunawajulisha kuwa kwa sasa hakuna mipira ya kondomu katika vituo vya afya ndani ya shule yetu."  Chuo hicho kiliandika katika memo kwa wanafunzi.

Chuo hicho kimetaadharisha wanafunzi  kujizuia wakiwa na uwezo, kuwa waaminifu kwa wapenzi wao na kujishughulisha katika mambo mengine wakati huu kunashuhudiwa uhaba wa kondomu.

Vile vile, wanafunzi wameshauriwa kununua bidhaa hizo madukani ikiwa watashindwa kujizuia ama watashindwa kuwa waaminifu katika mahusiano yao.