Watu 61 waliaga kwenye maandamano ya GenZ, Ripoti zaonyesha

Walitathmini video 45 na zaidi ya picha 100 zilizochukuliwa siku hiyo ya maandamano.

Muhtasari

• Ripoti hiyo imethibitisha kuwa visa 67 vya watu kuchukuliwa kwa nguvu  vilishuhudiwa, 40 wakiwa wameachiliwa huku 27 wakiwa bado hawajulikani waliko.

PRESS RELEASE
Image: HISANI

Takriban watu 61 walipoteza maisha yao wakati wa maandamano ya kupinga mswada wa fedha 2023/24.

Shirika la Amnesty International likishirikiana na mashirika mengine ya kutetea haki za kinadamu, limetoa ripoti inayoonyesha watu ambao walipoteza maisha yao katika maandamano hayo yalioanza Juni 25. 

Kulingana na ripoti hiyo 61 walipoteza maisha huku wengine 72 wakitekwa nyara au wasijulikane waliko kufuatia maaandamano hayo ambayo yaliendeshwa kwa njia ya amani.

Ripoti hiyo inashutumu polisi kwa kuzua vurumai kwa maandamano hayo. Ripoti hii imezinduliwa baada ya uchunguzi wa kina kufanywa na vile vile mahojiano kwa watu tofauti.

Mashirika hayo yalisema kwamba ripoti hiyo ilitokana na uchunguzi wa kina na ilijumuisha  kuhojiwa kwa mashahidi 23 wa matukio ya katika maandamano hayo.  Pia walitathmini video 45 na zaidi ya picha 100 zilizochukuliwa siku hiyo ya maandamano.

Kutokana na kanda hizo za video,wachambuzi hodari wa shirika hilo walisema kuwa katika siku hiyo, maafisa wa kudumisha amani walitumia nguvu kupita kiasi ili kuwatawanya waandamanaji kwa kutumia vitoza machozi,risasi halisi.

Ripoti hiyo imeonyesha kuwa watu sita waliuawa kwa kupigwa risasi. 

Vile vile,ripoti hiyo imethibitisha kuwa visa 67 vya watu kuchukuliwa kwa nguvu  vilishuhudiwa, 40 wakiwa wameachiliwa huku 27 wakiwa bado hawajulikani waliko.