DCI Amin azuru nyumbani kwa DJ Fatxo kabla ya mwili wa Jeff kufukuliwa Ijumaa

Amin aliwaagiza wapelelezi kufanya uchunguzi wa kina ili kuhakikisha ukweli na haki zimepatikana.

Muhtasari

•DCI ilisema Amin alifanya ziara hiyo kama sehemu ya uchunguzi unaoendelea wa kifo cha kutatanisha cha kijana huyo mwenye umri wa miaka 23.

•Uundaji upya wa eneo la tukio uliofanywa na timu ya upelelezi wa mauaji ya DCI ulilenga kubaini mapungufu katika kesi hiyo.

alipotembelea eneo la kifo cha Jeff Mwathi siku ya Jumatano, Machi 29.
Mkurugenzi wa DCI Mohamed Amin alipotembelea eneo la kifo cha Jeff Mwathi siku ya Jumatano, Machi 29.
Image: TWITTER// DCI

Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Bw Mohamed Amin, mnamo siku ya Jumatano alitembelea eneo ambapo marehemu Geoffrey 'Jeff' Mwathi alikumbana na kifo chake cha kusikitisha.

Katika taarifa yake ya Jumatano jioni, idara ya DCI ilisema Amin alifanya ziara hiyo kama sehemu ya uchunguzi unaoendelea wa kifo cha kutatanisha cha kijana huyo mwenye umri wa miaka 23.

Wakati huo huo, idara hiyo ilifichua kwamba shughuli ya ufukuzi wa mwili wa Mwathi itaendelea siku ya Ijumaa.

"Bw Amin alijiunga na timu ya wapelelezi wakati wa ujenzi upya wa eneo la tukio katika Redwood Apartment kabla ya kufukuliwa kwa mwili kulikoratibiwa siku ya Ijumaa, 31 Machi 2023," taarifa ilisoma.

Uundaji upya wa eneo la tukio uliofanywa na timu ya upelelezi wa mauaji ya DCI ulilenga kubaini mapungufu ambayo ufukuzi wa mwili unatarajiwa kutoa majibu punde tu uchanganuzi wa DNA na Sumu utakapokamilika.

Wakati wa ziara hiyo, Bw Amin alitoa changamoto kwa wapelelezi wanaohusika na kesi hiyo ambayo imekuwa ya kitaifa kufanya uchunguzi wa kina ili kuhakikisha kwamba ukweli na haki zimepatikana.

"DCI inawahakikishia familia na wanajamii kwamba hatimaye, haki itapatikana," taarifa ilisoma.

Siku ya Jumapili, Inspekta Jenerali wa polisi Japhet Koome alitangaza wapelelezi wanapanga kuufukua mwili wa marehemu Geoffrey Jeff Mwathi kama sehemu ya uchunguzi unaoendelea kuhusu kifo chake.

Koome alisema wamepata mapengo katika tukio hilo na hivyo wanahitaji kuufukua mwili wa marehemu ili kusaidia katika uchunguzi wao.

Alisema polisi wanaendelea na uchunguzi wa kina ili kuhakikisha haki inatendeka katika kesi hiyo.

"Tutafukua mwili huo kwa kuangalia vipimo vya mahali ambapo inasemekana alipita kwenye dirisha na kushuka hadi ghorofa ya chini. Tunaelekea kortini kutafuta agizo la uchimbaji wa kaburi hilo,” Koome alisema.

IG alibaini kuwa Jeff alizikwa zamani nyumbani kwao Nyandarua na hivyo kuna haja ya kutafuta agizo la kuufukua mwili huo.