Kunani? Safaricom yavunja kimya kuhusu hitilafu za intaneti kufuatia malalamiko ya umma

Kampuni hiyo imetahadharisha kuhusu uwezekano wa kasi iliyopungua ya mtandao kabla ya suluhu kamili kupatikana.

Muhtasari

•Kampuni ya Safaricom PLC imetoa taarifa kueleza kuhusu hitilafu ya mtandao iliyoshuhudiwa kuanzia siku ya Jumapili jioni.

•Safaricom ilikiri kukumbana na hitilafu kwenye moja ya kebo zinazotoa huduma ya intaneti ndani na nje ya nchi.

CEO PETER NDEGWA
Image: MAKTABA

Safaricom PLC, mtoa mkubwa wa huduma za simu na intaneti nchini Kenya imetoa taarifa kueleza kuhusu hitilafu ya mtandao iliyoshuhudiwa kuanzia Jumapili jioni.

Siku ya Jumapili jioni, Wakenya wengi walilalamika kuhusu kukatizwa kwa huduma za mtandao, jambo ambalo lilifanya iwe vigumu kwao kufanya kazi zinazohitaji huduma hizo

Kufuatia malalamiko hayo, kampuni hiyo inayotoa huduma za mtandao ilikiri kukumbana na hitilafu kwenye moja ya kebo zinazotoa huduma ya intaneti ndani na nje ya nchi, hatua iliyosababisha  tatizo hilo kushuhudiwa.

"Tumekumbana na hitilafu kwenye mojawapo ya nyaya za chini zinazotoa trafiki ya mtandao ndani na nje ya nchi," Safaricom ilisema kwenye taarifa.

Kuhusu hatua zilizochukuliwa kushughulikia suala hilo, kampuni hiyo ilisema "Tangu wakati huo tumeanzisha hatua za kupunguza shughuli ili kupunguza kukatizwa kwa huduma na kukuweka karibu tunapongojea urejeshaji kamili wa kebo."

Licha ya hatua zilizochukuliwa, kampuni hiyo hata hivyo ilitoa tahadhari kuhusu uwezekano wa kupungua kwa kasi ya mtandao kabla ya suluhu kamili kupatikana.

“Tunawashukuru kwa subira na uelewaji wenu,” walisema.

Taarifa hiyo ilifuatia malalamiko mengi kutoka kwa watumiaji wa mtandao nchini Kenya ambao walilalamika kuhusu kasi ya huduma hizo.

Maelfu ya Wakenya walitumia mitandao mbalimbali ya kijamii kuelezea masikitiko yao baada ya kukumbwa na matatizo katika kutumia huduma hizo.