Mwanawe Uhuru, Jomo afika mahakamani kupinga serikali kufutilia mbali leseni ya bunduki

Jomo Kenyatta anadai hajafahamishwa sababu za leseni yake kutiliwa mbali.

Muhtasari

• Mwanawe Rais wa Zamani Uhuru Kenyatta-John. J. Kenyatta ameiomba mahakama kuingilia kati na kukomesha serikali kumfutia leseni ya kumiliki silaha.

• Jomo Kenyatta anadai hajafahamishwa sababu za kufutwa kwa lengo hilo licha ya kuwa na leseni.

Mtoto wa Rais Uhuru Kenyatta Jomo Kenyatta akiwa na mkewe Fiona Achola.
Mtoto wa Rais Uhuru Kenyatta Jomo Kenyatta akiwa na mkewe Fiona Achola.
Image: HISANI

Mtoto wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, John Jomo Kenyatta ameelekea mahakama kuu kupinga uamuzi wa serikali wa kufutilia mbali leseni yake ya bunduki.

Katika ombi la dharura mbele ya Mahakama ya Milimani, mwanawe Rais wa Zamani Uhuru Kenyatta-John. J. Kenyatta ameiomba mahakama kuingilia kati na kukomesha serikali kumfutia leseni ya kumiliki silaha.

Jomo anamtaka afisa mkuu wa Bodi ya Leseni za silaha na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kusitisha ombi lake la kutaka kufutili mbali leseni yake ‘bila kufuata utaratibu uliowekwa katika Sheria ya Silaha’.

Katika barua yake ya mahakama, kupitia kwa Wakili Fred Ngatia, anasema uamuzi wa kunyang’anywa leseni yake ya kumiliki silaha ni kinyume na kifungu cha 5 (8) cha Sheria ya Silaha.

Anadai hajafahamishwa sababu za kufutiliwa mbali kwa leseni hiyo.

Jomo alisema maafisa walipokuja wakimtaka asalimishe bunduki zake mnamo Julai 21, hakuna sababu iliyotolewa.

"Nilipotaka kufahamu sababu kama zipo, zilizosababisha hatua hiyo ya ghafla, maafisa walijifanya kutojua," Jomo alisema.

Anadai hajafahamishwa sababu za leseni yake kutiliwa mbali licha ya kuwa na leseni.

"Sababu za kunyimwa leseni ya silaha zimetolewa katika kifungu cha 5(7) cha Sheria ya Silaha, ambacho kikisomwa na kifungu cha 7 (2) (a) (v) cha sheria ya utawala wa haki, hakiwezi kutumika bila kupewa fursa ya kusikilizwa," Jomo alisema.

Alisema endapo ombi lake halitakubaliwa kwa haraka ili kusikilizwa na amri zitakazotolewa, haki zake za kikatiba zitakiukwa.

Kulingana na hati za korti, leseni yake ni halali hadi Aprili 27, 2024.

Suala hilo bado halijasikilizwa.

Siku ya Ijumaa, Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki alisema bunduki 23 zilipatikana kutoka kwa nyumba tatu huko Karen, Nairobi, kufuatia operesheni iliyoanzishwa baada ya kubaini kuwa silaha zilizotumiwa wakati wa maandamo zilitolewa na watu waliokuwa na bunduki za kiraia.

"Leo alasiri, operesheni imekuwa ikiendelea kulenga nyumba tatu ndani ya eneo la Karen ambapo jumla ya bunduki 23, ambazo baadhi yake zinashukiwa kutumika katika shughuli haramu zimehifadhiwa," alisema Ijumaa.

Aliyekuwa rais Uhuru Kenyatta tangu wakati huo amejitokeza kutetea familia yake dhidi ya mashambulizi ya kuthubutu serikali kukabiliana naye ana kwa ana badala ya kuitetea familia yake.

Uhuru aliapa kutetea familia yake bila kujali gharama.