Wanaopeleka wasichana ughaibuni wako serikalini-Aisha Jumwa adai

Alitoa madai hayo Jumanne alipokuwa akihojiwa na Kamati ya Bunge ya Uteuzi.

Muhtasari
  • Alisema atakagua leseni za mashirika yanayopeleka wasichana Mashariki ya Kati
  • Alisema anaihurumia hali na familia za wale ambao wamepoteza wapendwa wao katika nchi za ughaibuni
AISHA JUMWA
Image: EZEKIEL AMING'A

Aliyekuwa Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa amedai kuwa watu wakuu serikalini ni sehemu ya mashirika yanayosafirisha wasichana wa Kenya hadi Saudi Arabia.

Alitoa madai hayo Jumanne alipokuwa akihojiwa na Kamati ya Bunge ya Uteuzi.

Jumwa ndiye mteuliwa wa Baraza la Mawaziri katika wizara ya Utumishi wa Umma na Hatua ya Kusimamia Jinsia.

"Watu wanaopeleka wasichana wetu ughaibuni ni watu wakubwa katika serikali yetu, na huo ushahidi upo," Jumwa alisema.

Alisema atakagua leseni za mashirika yanayopeleka wasichana Mashariki ya Kati.

Alisema anaihurumia hali na familia za wale ambao wamepoteza wapendwa wao katika nchi za ughaibuni.

Alisema iwapo itaidhinishwa, atafanya kazi kwa ushirikiano na Wizara ya Kazi na Wizara ya Mambo ya Nje kupitia upya leseni za mashirika yanayopeleka wasichanaughaibuni.

"Ni jambo la kusikitisha sana, kwanza kwa wazazi na familia ambazo zimepoteza ndugu zetu ambao wameenda kutafuta greener pastures  kule ughaibuni."

Alisema suala hilo litakuwa la kwanza atalishughulikia iwapo atapitishwa kuketi kwenye kizimbani.

Mbunge huyo wa zamani wa Malindi pia alisema atatengeneza nafasi nyingi za kazi kwa wasichana wa Kenya kwa hivyo hawatahitaji kwenda kutafuta malisho ya kijani kibichi katika ulimwengu wa Kiarabu.

Jumwa aliongeza kuwa pia atahakikisha wasichana hao wanapata sehemu ya mapato kutoka kwa Mfuko wa Hustler wa Sh50 bilioni ili kuanzisha biashara na kujiajiri.

Visa vya wasichana kudhalilishwa na hata kuuawa katika Mashariki ya Kati vimeongezeka katika siku za hivi karibuni.