'Muombe Miguna Miguna msamaha,'Karua amwambia Rais Ruto

Karua aliendelea kuelezea kufukuzwa kwa Miguna kama kinyume cha sheria

Muhtasari
  • Kulingana naye, Miguna alifurushwa na utawala wa Jubilee ambapo Ruto alihudumu kama naibu rais
KIongozi wa NARC aandika mistari ya wimbo wa kuhimiza
Martha Karua, KIongozi wa NARC aandika mistari ya wimbo wa kuhimiza
Image: Twitter

Kiongozi wa chama cha Narc-Kenya Martha Karua sasa ana maoni kwamba Rais William Ruto ndiye anafaa kuwa wa kwanza kumwomba msamaha wakili Miguna Miguna kuhusu kufukuzwa kwake 2018.

Karua anasema kwamba Mkuu wa Nchi alichangia katika masaibu yaliyompata wakili huyo takriban miaka mitano iliyopita, na hapaswi kuchukuliwa kuwa alithibitisha matendo yake baada ya kuwezesha kurejea kwake siku ya Alhamisi.

Kulingana naye, Miguna alifurushwa na utawala wa Jubilee ambapo Ruto alihudumu kama naibu rais, hivyo basi anapaswa kubeba mzigo wa kuomba msamaha kwa bosi wake wa wakati huo na sasa mtangulizi Uhuru Kenyatta.

"Kilichotokea kilikuwa kosa kubwa na ukatili wa serikali ya Kenya ambayo rais wa sasa alikuwa naibu wa rais mwenye furaha wakati huo," Karua alisema katika mahojiano na BBC News.

"Ni kitendo ambacho hawezi kujitenga nacho. Kwa kweli, leo ningetarajia angeomba msamaha kwa Miguna kwa niaba yake na kwa niaba ya Rais ambaye amestaafu. Ni serikali yao iliyofanya unyama huo. ”

Karua aliendelea kuelezea kufukuzwa kwa Miguna kama kinyume cha sheria akisema kwamba ikiwa chama cha muungano cha Azimio la Umoja One Kenya kinachoongozwa na Raila Odinga kingenyakua urais kwenye uchaguzi wa Agosti, basi wangemruhusu wakili huyo kurejea Kenya.

“Kampeni yetu ilikuwa chini ya jukwaa la utawala wa sheria, uzingatiaji wa katiba na wengi wanaweza kukumbuka, Raila Odinga alikuwa amedokeza kwamba ningeshughulikia maswala ya katiba na sheria. Miguna angeweza kufurahia haki zake na kurejeshewa pasipoti yake," Karua, ambaye alikuwa mgombea mwenza wa Odinga, alisema.

Miguna aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) Alhamisi asubuhi.