Ukimfungia Raila nje ya ulingo wa siasa, ataugua - Mbunge James Gakuya

Gakuya alisema kuwa siasa ni kama chakula kwa baadhi ya viongozi na kuwafungia nje ni kama kuwatesa kwa njaa.

Muhtasari

• Kama kwa mfano ungemzuia kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kufanya siasa, angeugua. - Gakuya alisema.

Raila Odinga
Image: RAILA ODINGA/TWITTER

Licha ya kushindwa katika kinyang'anyiro cha urais cha Agosti 9, Raila Odinga amerejea katika ulingo wa kisiasa nchini. Kando na Odinga, Wakenya kila mara wamekuwa wakionyesha msisimko kila wanapomwona Uhuru Kenyatta hadharani baada ya kukabidhi mamlaka.

Mbunge wa Embakasi Kaskazini James Gakuya amebainisha kwamba wanasiasa hao wawili – Kenyatta na Odinga wana umuhimu wao na nafasi pia katika siasa za Kenya, hata baada ya Kenyatta kustaafu baada ya kukabidhi madaraka kwa rais mpya William Ruto.

Akizungumza katika kituo cha runinga ya NTV, mbunge huyo siasa ni mzunguko wa kila siku na katu haziwezi zikaisha. Pia alisema kwamba ni vigumu sana kwa taasisi au vyombo vya dola kumfungia mwanasiasa yeyote ili kutozungumza mawazo yake kwani wengine wana uzoefu mkubwa na ukiwafungia ni sawa na kuwatesa njaa.

Mbunge huyo ambaye alionekana kulinganisha siasa na chakula alisema mwanasiasa siku zote ni kama mpishi kwani hawezi kosa kupatikana jikoni.

“Hakuna siku mwanasiasa atakosa kupatikana jikoni, na huwezi ukamfungia mwanasiasa kujieleza kwa umma kila mara,” Gakuya alisema.

Alitolea mfano kuwa kwa uzoefu alionao, kiongozi wa ODM Raila Odinga hawezi kufungiwa kutozungumza kwani kufanya hivo ni sawasawa na kumtesa njaa na kutaka afe.

“Kama kwa mfano ungemzuia kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kufanya siasa, angeugua. Yeye ni mwanasiasa, na damu yake ni siasa. Hata Rais mstaafu Uhuru Kenyatta tunavyozungumza popote alipo anaumwa kwa kuwa yuko mbali na ulingo wa siasa. Nadhani siasa zisizoharibu nchi ni afya” Gakuya alieleza.