Sakaja asema vijana watalipwa Sh2500 kwa wiki kwa kupanda miti

Aliongeza mradi huo pia utasaidia kupunguza uhalifu kwani vijana watakuwa na kazi ya kufanya.

Muhtasari
  • Hii si mara ya kwanza kwa Gavana huyo kusisitiza haja ya kupanda miti jijini
Gavana wa Nairobi , Johnson Sakaja
Gavana wa Nairobi , Johnson Sakaja
Image: Facebook

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja amesema vijana watalipwa Sh2500 kila wiki katika mpango wa upandaji miti ambao haujaanza.

Sakaja alisema kutokana na Kazi Mtaani iliyoondolewa na Rais William Ruto, inabidi programu ianzishwe ili kuwafanya vijana kuwa na shughuli nyingi na kuwawezesha kujikimu kimaisha.

“Tulikubaliana na Rais wetu kuwa vijana tunaozingatia, badala ya tuliokuwa nao kazi mtaani, hivi karibuni tunazindua mpango wa upandaji miti.

"Vijana wetu watajishughulisha na watakuwa wakipata Sh25oo kwa wiki. Watatusaidia kupanda miti na kutunza miti," alisema.

Aliongeza mradi huo pia utasaidia kupunguza uhalifu kwani vijana watakuwa na kazi ya kufanya.

Hii si mara ya kwanza kwa Gavana huyo kusisitiza haja ya kupanda miti jijini.

Mnamo Oktoba, Sakaja alisema kutakuwa na zoezi mwafaka la upandaji miti ambalo litafanywa na kaunti na sekta ya kibinafsi.

Akizungumza wakati wa kukabidhi huduma za Nairobi Metropolitan Services kwa kaunti hiyo, Sakaja alisema itakuwa katika jitihada za kuleta Nairobi juu na zaidi ya hadhi nzuri katika jiji ilivyokuwa hapo awali.

"Ukipanda KICC, ambayo ni afisi yangu ya zamani, na ukitazama pande zote, unaona kanda tatu za kiikolojia, kuna upande wa kijani kibichi, kisha kuna upande wa kahawia halafu kuna upande unaofanana na jangwa."

"Lazima tupange miti katika jiji na kurudisha utukufu wake; mji wa kijani kibichi," alisema.