(+video) Maajabu kondoo wakizunguka mduara zaidi ya siku 12 mfululizo bila kuchoka

Majarida ya kimataifa yalisema kuwa huo huenda ni ugonjwa kwa jina Listeriosis unaosababisha kuzunguka kwa wanyama.

Muhtasari

• Picha zilizopigwa wiki mbili zilizopita kaskazini mwa Uchina, zinaonyesha mamia ya kondoo wakifuatana kwenye duara kubwa.

Ukistaajabu ya Musa, basi itakuwa hujayaona ya Firauni na fimbo yake!

Nchini Uchina, kuna video moja ambayo imezua gumzo pevu kote duniani. Video hiyo inaonesha makumi ya kondoo wakitembea kwa mzunguko wa dura pasi na kusita.

Kulingana na video hiyo fupi iliyopakiwa na jarida la People's Daily la China, inaonesha kondoo hao weupe wakitembea kwa kuzunguka mduara huku wengine wakionekana kuchoka ila bado safari ya mzunguko inaendelea.

“Siri kubwa ya kondoo! Mamia ya kondoo watembea kwenye duara kwa zaidi ya siku 10 huko N Mongolia ya Ndani ya Uchina. Kondoo hao wana afya nzuri na sababu ya tabia ya ajabu bado ni siri,” People's Daily la Uchina waliandika kwenye video hiyo.

Jarida la Metro la nchini Uingereza liliripoti kuwa kondoo hao walionesha tabia hiyo isiyo ya kawaida na kuwa wamekuwa wakizunguka kwa zaidi ya siku 12 sasa bila kusita.

“Picha zilizopigwa wiki mbili zilizopita kaskazini mwa Uchina, zinaonyesha mamia ya kondoo wakifuatana kwenye duara kubwa. Mmiliki wa kondoo, Bi Miao anadai ilianza na kondoo wachache kabla ya kundi zima kujiunga. Katika video, kondoo wengine wanaweza pia kuonekana wamesimama kabisa, lakini bado wanadumisha umbo la mviringo,” Metro waliripoti.

Inasemekana kuna zizi 34 za kondoo mahali hapo, lakini ni kondoo tu katika zizi la nambari 13 walioonekana kuwa na mwenendo huu wa kustaajabisha.

“Ingawa haijulikani kwa hakika ni nini kilisababisha kondoo kufanya hivi, ugonjwa wa bakteria uitwao Listeriosis umejulikana kusababisha ‘kuzunguka’ kwa wanyama,” jarida hilo lilifichua.