Lazima tusimame na wakulima wetu-Hisia za Sifuna baada ya mjadala mkali kuhusu mahindi ya GMO

Alisema vita hivyo ni sawa na vilivyoshuhudiwa miaka kadhaa iliyopita kati ya wakulima wa sukari na waagizaji wa bidhaa hiyo ya thamani.

Muhtasari
  • Kuporomoka kwa viwanda vya sukari nchini Kenya kulichangiwa pakubwa na uagizaji wa sukari bila ushuru
Mgombea wa useneta wa Nairobi Edwin Sifuna wakati wa kibali Kasarani.
Mgombea wa useneta wa Nairobi Edwin Sifuna wakati wa kibali Kasarani.

Huku mjadala mkali kuhusu mahindi ya GMO ukizidi kupamba moto mitandaoni Edwin Sifuna ametoa hisia zake na kudai kwamba lazima Wakulima wa mahindi nchini waungwe mkono.

Katika taarifa yake Jumanne, seneta huyo alidai suala la msingi ni masilahi ya kibiashara ya wafanyabiashara wa upande mmoja na wakulima wa mahindi kwa upande mwingine.

"Mjadala wa GMO hauhusu usalama wa chakula. Ni mpaka mpya wa vita hivi kati ya wakulima na wafanyabiashara," Sifuna alisema.

Alisema vita hivyo ni sawa na vilivyoshuhudiwa miaka kadhaa iliyopita kati ya wakulima wa sukari na waagizaji wa bidhaa hiyo ya thamani.

"Vita vya kibiashara kati ya wakulima na wafanyabiashara vimeendelea kwa miaka mingi katika ukanda wa Sukari. Cha kusikitisha ni kwamba wakulima wa sukari walipoteza hiyo. Ni lazima tusimame na wakulima wetu wa mahindi," Sifuna alisema.

Kuporomoka kwa viwanda vya sukari nchini Kenya kulichangiwa pakubwa na uagizaji wa sukari bila ushuru nchini kutokana na ushindani usio wa haki.

Ripoti iliyoeleza kwa kina watu waliohusika na uagizaji wa sukari nchini kinyume cha sheria ilikuwa Agosti 9, 2018, ilipopigiwa kelele na wabunge walioshutumu jopo kazi lililoongozwa na Mbunge wa Kieni Kanini Kega kwa kufanya kazi mbaya.