Bora uhai siasa baadaye!Moses Kuria asema huku mjadala mkali kuhusu mahindi ukiendelea

Kuria aliongeza kuwa vitendo vyake havina nia ya kuwakandamiza wakulima wa Kenya

Muhtasari
  • Moses alikariri lengo lake la kupunguza gharama ya maisha na kuzuia njaa miongoni mwa Wakenya
MOSES KURIA
Image: EZEKIEL AMING'A

Waziri wa Biashara Moses Kuria amekuwa akipokea kejeli utoka kwa wakenya  baada ya kufichua mpango wa serikali wa kuagiza magunia milioni 10 ya mahindi.

Kuria alisema kuwa mahindi yasiyotozwa ushuru ambayo yataagizwa kutoka nje kwa muda wa miezi sita ijayo yatajumuisha Marekebisho ya Jeni (GMO) na yasiyo ya GMO.

Baada ya ghasia kuhusu usalama wa mahindi hayo, Waziri huyo alipuuzilia mbali wakosoaji akisema mahindi ya GMO yanaweza kuongezwa kwenye orodha ya mambo yanayoweza kuua Wakenya.

Kuria amekuwa akikashifiwa kwa kauli zake, huku viongozi sasa wakimtaka aombe radhi, la sivyo, mchakato wa kuondolewa kwake utaanza.

Kupitia ukurasa wake rasmi wa twitter Jumanne jioni, Moses alikariri lengo lake la kupunguza gharama ya maisha na kuzuia njaa miongoni mwa Wakenya.

Kuria aliongeza kuwa vitendo vyake havina nia ya kuwakandamiza wakulima wa Kenya na kwamba hajapendezwa na siasa zinazohusu uagizaji wa mahindi kutoka nje ya nchi.

“Serikali ilifanya kampeni kwa ahadi ya Kupunguza gharama ya maisha na kuhakikisha hakuna Mkenya anayekufa kwa njaa. Hili ni jukumu letu la msingi la umoja na la pamoja na kiwango cha chini kisichoweza kupunguzwa. Tutafanya hivyo hasa tunapolinda maslahi ya wakulima. Bora uhai, siasa baadaye!”Kuria  aliandika.

Kauli yake  imejiri saa chache baada ya Wabunge kutoka mikoa inayolima mahindi kufanya mkutano na waandishi wa habari bungeni, ambapo walimkashifu kwa hatua ya kuagiza mahindi ya GMO na yasiyo ya GMO.