Atwoli atofautiana na Raila kuhusu Ruto kuwa dikteta

Atwoli alieleza kuwa wafanyakazi wengi wako katika sekta isiyo rasmi na bila amani nchini hawataweza kujikimu kimaisha.

Muhtasari
  • Akizungumza Jumamosi, Novemba 26, Atwoli alisema kuwa nchi iko mbali na kuwa taifa la kiimla
Bosi wa COTU Francis Atwoli
Bosi wa COTU Francis Atwoli
Image: MAKTABA

Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU) Francis Atwoli ametofautiana na kiongozi wa chama cha Muungano wa Azimio One Kenya Raila Odinga kwa madai kwamba Rais William Ruto anakuwa dikteta.

Akizungumza Jumamosi, Novemba 26, Atwoli alisema kuwa nchi iko mbali na kuwa taifa la kiimla.

"Sisi si taifa la kidikteta, hatujakaribia huko," Atwoli alizungumza.

Katibu huyo alisema kwamba viongozi wa kisiasa wanaomkashifu Ruto wanapaswa kupewa uhuru wa kufanya hivyo akitaja kuwa ni afya kwa demokrasia ya taifa.

"Wanaosema Ruto ni dikteta ni viongozi katika nafasi za kisiasa, waache waongee kwa sababu ndivyo walivyopigania," akaeleza.

Atwoli ambaye alikuwa mkosoaji mkali wa Ruto katika maandalizi ya uchaguzi alienda kumsifu katika hali ambayo haikutarajiwa.

"Serikali hii ya sasa imekuza uhuru wa kujieleza, rais hajamkashifu yeyote kwa kumkosoa," Atwoli alimsifu Ruto.

Alienda mbali zaidi na kuwaonya wanasiasa kutotoa matamshi yanayoweza kuvuruga amani nchini.

"Wacha watu waseme wanachotaka kusema lakini sisi si nchi ya kidikteta na wanapaswa kuhakikisha kuwa matamshi yao hayavurugi amani tunayofurahia sasa," alionya.

Atwoli alieleza kuwa wafanyakazi wengi wako katika sekta isiyo rasmi na bila amani nchini hawataweza kujikimu kimaisha.