Wakenya wafurahishwa jinsi DP Gachagua alishambulia mahindi choma (Video)

Wengi walisema kuwa naibu rais ni mkweli kwani hana muda wa kuficha tabia yake, anaionesha jinsi ilivyo hadharani.

Muhtasari

• “Kusema tu ukweli Riggy G ndiye anafaa kuitwa Hasla wa kweli,” Ammar Kassim aliandika Twitter.

Jumatano rais Uhuru Kenyatta, naibu wake Rigathi Gachagua na wanasiasa wengine pamoja na wafanyibiashara mbalimbali walihudhuria hafla ya uzinduzi wa mkopo wa Hasla jijini Nairobi.

Katika uzinduzi huo, viongozi hao walitembelea biashara mbalimbali za wapambanaji waliokuwa wakionesha biashara yao.

Rais Ruto na naibu wake walifika kwa mwanaume mmoja mchuuzi wa mahindi choma na walinunua bidhaa hiyo kama njia moja ya kuunga mkono biashara za wapambanaji.

Wawili hao walianza kushambulia mahindi yale lakini katika video ambazo zimekuwa zikisambaa mitandaoni, naibu rais Rigathi Gachagua alionekana kusahau kuwa watu walikuwa wanamtazama.

DP Gachagua alishambulia mahindi kweli kweli bila woga wala kuremba, jambo ambalo lilizua vichekesho na utani mwingi mitandaoni, Wakenya wakimsifu jinsi alivyo mkweli bila kuigiza akiwa hadharani kwani yeye huonesha tabia yake ya faraghani peupe.

Wengine walisema Gachagua ndiye mtu halisi anayefaa kupewa jina la Hasla wa kweli kwani kwa kasi ile ambayo alikuwa akishambulia mahindi choma kwa meno basi kunaonesha mpendwa naibu wa rais alikuwa na njaa kweli.

“Kusema tu ukweli Riggy G ndiye anafaa kuitwa Hasla wa kweli,” Ammar Kassim aliandika Twitter.

“Ikiwa hujawahi kumpenda DP wetu Riggy G lazima uwe nje ya ulimwengu huu. Rigathi kamwe hajifanyi. Alishika mahindi choma na kufurahia shoo hiyo. Nyinyi endelea kusema hustler fund,” Kawangware Finest alisema.