Mark Masai akana madai ya kufutwa kwa sababu ya HR mwanamke

Masai alisema kuwa si kweli ila wengi wakataka kujua zaidi ya hapo.

Muhtasari

• Mtumizi wa Twitter ndiye aliyeanzisha gumzo hilo kwa kusema kuwa alifutwa kazi baada ya kuzozana na HR wa kike.

Mwanahabari Mark Masai
Mwanahabari Mark Masai
Image: FaCEBOOK

Aliyekuwa mwanahabari wa kituo cha runinga cha NTV Mark Masai amejitokeza na kupuuzilia mbali madai kuwa kibarua chake kiliota nyasi kutokana na kuzorota kwa uhusiano baina yake na HR mmoja mwanamke katika kampuni ya NMG.

Madai hayo yalianzishwa kweney mtandao wa Twitter na mtu mmoja kwa jina Drey Mwangi ambaye alisema kuwa Masai ni mwanahabari mzuri lakini inasikitisha safari yake ya kuitumikia runinga hiyo ililazimika kukatishwa kwa sababu ya mwanamke anayefanya kitengo cha HR.

“Mark Masai mwanamume ambaye ni mzuri sana katika kazi yake anafukuzwa ghafla kutoka NTV, kwa sababu ya mwanamke HR,” Drey Mwangi aliandika.

Masai alidamka kwa haraka na kunyoosha maelezo ambapo alisema kwa maelezo machache kuwa si kweli hata ncha.

“Si kweli Drey Mwangi,” Masai aliandika.

Mwanahabari huyo nguli aliachishwa kazi hivi majuzi kutoka kampuni ya Nation Media Group (NMG) baada ya miaka 14, na amekuwa mstari wa mbele kukanusha uvumi unaoenea kuhusu kufukuzwa kwake kutoka NTV.

Hata hivyo mwanzishilishi wa gumzo hilo kwenye Twitter, Drey Mwangi hakuridhika na majibu hayo ya Masai na kumtaka kuwaelezea watu hadithi kwa mapana kwani Twitter ni sehemu yenye usalama mtu kuzungumza ukweli wake.

Wengine walichukua fursa hiyo kutoa madhira yao jinsi walijipata pagumu na wanawake HR katika afisi mbalimbali.

“Mark, tuambie hadithi kamili au tutalipua kutoka kwa vyanzo vyetu vya kuaminika,” mmoja alimwambia.

“Mark uko na uhakika si eti unamtetea HR?” Mwingine alitaka kujua.