Sarah Cohen atembelea kaburi la mumewe, siku chache baada ya kesi ya mauaji kuondolewa

Sarah alionekana akiwa na koja la maua ambayo aliyaweka kwa umakini juu ya kaburi hilo kabla ya kuwa na kimya cha sekunde kadhaa.

Muhtasari

• DPP alituma ombi la kutaka kuondolewa kwa mashtaka dhidi yake kufuatia kukosekana kwa ushahidi wa kumtia hatiani.

• Tangu mwezi Januari mwaka 2020, Sarah amekuwa akizuru kaburi la mumewe na maua mara kwa mara.

Mjane Sarah Cohen akiwa kwenye kaburi la mumewe Tob Cohen
Mjane Sarah Cohen akiwa kwenye kaburi la mumewe Tob Cohen
Image: Hisani

Alhamisi mchana, Sarah Cohen, mke wa tajiri Mholanzi Tob Cohen aliyefariki miaka mitatu iliyopita kwa njia tatanishi alitembelea makaburi ya Kiyahudi jijini Nairobi alikozikwa Mholanzi huyo.

Katika picha ambazo zimesambazwa mitandaoni, Sarah alionekana akiwa na koja la maua mikononi ambapo alilitwaa kwa umakini juu ya kaburi la Cohen kabla ya kufanya ishara ya kimya cha dakika kadhaa, kama ambavyo huwa anafanya kila mara anapotembelea kaburi la marehemu mume wake.

Mumewe Cohen alipatikana amefariki huku mwili wake umerundikwa kwenye tundu la choo cha ndani nyumbani kwake mwaka 2019 ambapo familia yake kutoka Uholanzi imekuwa ikifuatilia kwa ukaribu kesi dhidi ya mauaji yake – mkewe Sarah Cohen akitajwa katika kesi hiyo kama mshukiwa mkuu.

Mapema wiki hii, mahakama ilitupilia mbali kesi ya mauaji ya Tob Cohen dhidi ya Sarah kwa ukosefu wa ushahidi.

Mashtaka dhidi yake yaliondolewa kufuatia ombi la mkurugenzi wa mashtaka ya umma Noordin Haji aliyetaka kesi hiyo kuondolewa kwa kukosekana ushahidi wa kutosha kumtia hatiani mwanamke huyo.

Uondoaji huo ulikuja siku chache baada ya mjane wa Cohen kumshutumu aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI), George Kinoti, kwa kubuni ushahidi katika kesi ya mauaji ya Cohen. Alidai kuwa hakupata nafasi ya kuomboleza kifo cha mumewe kwa sababu alisukumwa pande tofauti huku uchunguzi wa mauaji ya mumewe ukichukua mkondo huo. "Bado naomboleza kifo cha mume wangu. Sijawahi kupewa nafasi ya kumuomboleza mume wangu; nimerushwa kutoka upande mmoja hadi mwingine," alisema baina ya majonzi.

Mjane huyo alisema kuna sababu ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (ODPP) kufanya uchunguzi zaidi kwa sababu kuna zaidi ya inavyoonekana. Alidokeza kuwa watu wanaowaamini kama familia kuwasaidia walikuwa na shughuli nyingi za kutunga uwongo ili kubadili kesi hiyo kwa njia ambayo ingewanufaisha wao na si kutafuta haki inavyopaswa kuwa.