Mashujaa Dei: Fahamu Historia ya nyimbo za Kizalendo Kenya, kila kitu unafaa kujua

Nyimbo hizi za kizalendo zinawakumbusha Wakenya mapambano ya kunyakua uhuru kutoka kwa mabepari.

Muhtasari

• Nyimbo hizi za kizalendo zinatoa mafunzo na wosia wa kudumu kwa Wakenya kuipenda nchi yao na kujihisi fahari kuwa miongoni mwa taifa hili.

• Kenya ilijinyakulia uhuru mwaka wa 1963 kutoka kwa Wakoloni Waingereza baada ya mapambano ya muda mrefu yaliyogharimu maisha ya jasiri wengi.

Bendera ya Kenya
Bendera ya Kenya
Image: Bendera ya Kenya

Kila mwaka Oktoba 20, Kenya imekuwa ikisherehekea siku ya kitamaduni ya Mashujaa, awali ikiitwa Kenyatta Dei, siku ambayo taifa la Kenya tunakumbuka mashujaa wengi waliojitoa kwa hali na mali kuipambania bendera ya Kenya ili kutunyakua kutoka mikono ya mabepari wakoloni.

Tangu mwaka 1963, Wakenya walifurahia kupata uhuru wao na wengi walionesha furaha yao kupitia nyimbo za kizalendo na kishujaa – kwani wataalam wanasema nyimbo ndio njia pekee ya kuzungumza hisia za ndani – iwe furaha, huzuni na hisia zingine zote.

Oktoba 20 hii ikiwa ni siku ya Mashujaa, Radio Jambo tunazamia zaidi baadhi ya nyimbo za kizalendo ambazo zilivuma miaka ya nyuma na ambazo mpaka sasa zinavuma kutukumbusha kama Wakenya umuhimu wa kujivunia uhuru wetu kutoka kwa Wazungu – Uhuru ambao haukuja bure ila kwa ncha ya upanga, mateso makali msituni na katika vizuizi vya wakoloni ambayo vikundi kama Mau Mau walipitia ilmradi Kenya iwe huru.

Baadhi ya nyimbo hizo ni kama;

  1. Kenya nchi yangu - Kakai Kilonzo

Kakai Kilonzo aliachia kibai hiki mwaka wa 1983, alikuwa mwanamuziki kutoka Kilimanbogo, Wilaya ya Machakos, Kenya. Alikuwa kiongozi wa bendi ya Kilimambogo Brothers kuanzia 1975 hadi kifo chake mwaka 1987. Kilonzo aliimba kwa Kamba na Kiswahili.

2. Harambe harambee - Daudi Kabaka

Kabaka mpaka leo hii hajatokea mwanamuziki mwingine wa kutunga nyimbo aina ya Twist kama yeye. Aliachia kibao hiki mwaka wa 1982 akiwarai Wakenya kushirikiana kwa pamoja ili kuvuta maendeleo kwa faida ya wote.

3. Tushangilie Kenya - Mwalimu Thomas Wesinga

Mwalimu Wesonga ni mkongwe na mtunzi wa nyimbo za kizalendo ambaye alikuwa anaongoza kwaya mbalimbali katika nyimbo za mashindano ya kitaifa. Kwa sasa, anafanya kazi na kikosi cha utunzi wa miziki ya kizalendo cha PPMC.

4. Najivunia kuwa Mkenya - Avril & Trupee

Wasanii hao walikuja pamoja mwaka 2011 na kutunga wimbo wa kuonesha furaha na faraja yao kuwa miongoni mwa Wakenya wanaofurahia Amani ya kudumu na ardhi yenye rotuba nzuri ya kufanya ukulima

5. Daima Mkenya - Eric Wainaina

Wainaina ni Mkenya ambaye umaarufu wake ulikuja kutokana na tungo za kizalendo kama hii moja ambayo inasimulia uzuri wa Kenya kupitia rangi nne za bendera yetu.

6. Mungu baba twaomba - Rufftone & GSU

Rufftone ni msanii mkongwe wa nyimbo za injili ambaye aliungana na kwaya ya kikosi cha maafisa wa GSU kuimba wimbo wa kutaka Mungu kuleta Amani Kenya haswa baada ya machafuko ya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007-08.

7. Shukuru Mungu – Kidum

Msanii mkongwe kutoka pwani ya Kenya. Wimbo huu anawausia Wakenya muda wote kuwa na shukrani wanapoona Amani na utulivu vimetanda kote kwani kuna mataifa mengine mengi ambayo hayajawhi onja uzuri wa uhuru na Amani, kwani lugha ya vita na machafuko ndiyo wanazaliwa na kufa nayo.

8. Wakenya pamoja - Wasanii wa Kenya

Mtayarishaji wa muziki R.Kay aliwaleta pamoja wasanii wa Kenya kutoka pande mbalimbali za muziki kwa wimbo huu unaokuza umoja nchini.

9. Wimbo wa historia – Leyla Mohammed

Mwanafunzi wa miaka 13 kutoka Eastleigh ameipa wimbo wa kizalendo wa ‘Wimbo wa Historia’ maisha mapya. Wimbo huu unajulikana haswa kwa sauti yake ya mhemko katika kuelezea hadithi za Kapenguria Six, haswa Mzee Jomo Kenyatta.

Ungo hii iliandikwa katika miaka ya 1970 Enock Ondego na iliimbwa kwa mara ya kwanza na wanafunzi wa shule ya msingi kwa Rais Jomo Kenyatta katika ziara yake ya Taita Taveta.

10. My land is Kenya - Roger Whittaker

Wimbo huu ulitoka na kusikilizwa kwa mara ya kwanza mwaka 1982 na unasimulia uzuri wa Kenya huku akiwaambia watu kuwa wanaweza kutembea kote duniani lakini hakuna sehemu itakayofanana na Kenya, iwe kwa mabaya au mazuri.