Chebukati ni mtu muwazi sana, anafaa kuwa rais baada ya Ruto - Mchungaji Timothy Njoya

Mchungaji huyo alimsifia Chebukati kwa kuendesha uchaguzi wa haki na uwazi licha ya majaribio mengi ya ushawishi.

Muhtasari

• Chebukati ndiye Mkenya shupavu zaidi, muwazi (kama mtoto), asiye na hatia (kama mtoto)   - Njoya alisema.

Mchungaji mstaafu wa PCEA Timothy Njoya ampigia debe Chebukati kuwa rais ajaye
Mchungaji mstaafu wa PCEA Timothy Njoya ampigia debe Chebukati kuwa rais ajaye
Image: Maktaba

Mchungaji mmoja nchini kwa jina Timothy Njoya ameibuka na usemi unaoegemea kisiasa zaidi kuliko kuwahubiria watu kuhusu ufalme wa mbinguni.

Mchungaji huyo kupitia ukurasa wake wa Twitter alizua mgawanyiko baina ya waumini wake alipomsifia mwenyekiti wa tume huru ya mipaka na uchaguzi IEBC Wafula Chebukati katika kile alisema kuwa ni mtu muungwana sana ambaye anafaa kuwa rais wa Kenya wakati mmoja kabla kutamatika kwa maisha yake duniani.

Njoya alimsifia Chwebukati kwa kusimama imara dhidi ya vitisho kutoka kwa baadhi ya watu wenye ushawishi mkubwa katika setkali iliyopita na kuendesha uchaguzi kwa njia ya haki na kweli.

Kulingana na mwanaharakati huyo mkongwe, Chebukati alionyesha ujasiri na uthabiti katika kutangaza matokeo ya uchaguzi wa urais baada ya Wakenya kupiga kura Agosti 9.

Hata hivyo aliwaonya Rais William Ruto na wafuasi wa Raila Odinga kutokerwa na wadhifa wake kwani haukuelekezwa kwao kama hadhira.

“Chebukati ndiye Mkenya shupavu zaidi, muwazi (kama mtoto), asiye na hatia (kama mtoto), anayeaminika na mwenye msimamo thabiti wakati huu wa Karne ya 21 ambaye anafuzu kuwa Rais ajaye wa Kenya. Tathmini yangu ya Chekubati si ya kuchukuliwa na wapambe wa Ruto na Raila,” Njoya alisema.

Watu kwenye mtandao wa Twitter walimshambulia kwa njia tofauti, baadhi wakiunga mkono maneno yake na wengine wakimkashfu vikali kuwa hafai kuingilia masuala ya kisiasa bali anafaa kubaki katika kuwaonesha watu njia ya kuupata wokovu.

“Mtumishi wa Mungu, tafadhali usitufanye tuanze kujenga chuki dhidi ya watumishi wa Mungu bila sababu,” Sam Sagwe alimuomba.

“Ikizingatiwa kuwa alisimama tisti pasi na kuyumbishwa na mtu yeyote ni jambo la kumsifia, pia yeye ni mwanadamu ambaye hajakamilika lakini alifanya kazi kuzidi matarajio ya wengi,” Gichinga Side alisema.