Gavana Mwangaza atokwa na machozi baada ya Seneti kumuokoa

Gavana alikuwa katika vyumba vya seneti wakati uamuzi wa mwisho uliposomwa.

Muhtasari
  • Mnamo Jumanne, Kawira alikana mashtaka mbele ya kamati maalum akisema ni mwathiriwa wa uhuni

Gavana wa Meru Kawira Mwangaza alishindwa kuzuia machozi yake baada ya Kamati ya Seneti kutupilia mbali mashtaka dhidi yake.

Mwangaza alifuta machozi huku mwenyekiti wa jopo hilo Seneta wa Kakamega Boni Khalwale akisoma uamuzi huo.

Gavana alikuwa katika vyumba vya seneti wakati uamuzi wa mwisho uliposomwa.

Jopo hilo lilihitimisha vikao vyake Jumatano kabla ya kurejea kuandika uamuzi wake.

Kawira alitimuliwa mnamo Desemba 14 na MCAs 67 kati ya 69 waliokuwa kwenye Bunge la Kaunti ya Meru.

Wawakilishi wa kata walimshtumu gavana huyo kwa utovu wa nidhamu na matumizi mabaya ya ofisi, yote yakigawanywa kwa mashtaka matano.

Mnamo Jumanne, Kawira alikana mashtaka mbele ya kamati maalum akisema ni mwathiriwa wa uhuni.

MCAs walimshtumu kwa kufanya angalau ukiukaji wa katiba katika kila siku 64 ambazo amekuwa mamlakani.

Kupitia kwa wakili Muthomi Thiankolu, bunge hilo lilisema kulikuwa na ukiukaji wa Katiba 62, wote ulifanyika ndani ya siku 64.