Kampuni ya Canada, Iristel kujiunga na Safaricom, Airtel na Telkom katika soko la Kenya

Kenya itakuwa taifa la kwanza Afrika ambapo Iristel itaanzisha huduma zake.

Muhtasari

• Mwaka jana, Safaricom walipanua huduma zao za mawasiliano katika taifa jirani la Ethiopia.

Kampuni ya mawasiliano ya Iristel kuingia katika soko la Kenya
Kampuni ya mawasiliano ya Iristel kuingia katika soko la Kenya
Image: Twitter

Kampuni ya mawasiliano kutoka Canada kwa jina Iristel imetangaza mipango yake ya kuleta ushindani katika soko la Kenya ili kujiunga na makampuni mengine kama Safaricom, Airtel na Telkom.

Iwapo mipango hiyo yao itafanikishwa, kampuni hiyo ya kimataifa itakuwa imewekeza Kenya kama taifa la kipekee katika bara la Afrika, kwani hakuna taifa la Afrika ambalo tayari wanatoa huduma zao.

Kulingana na jarida la Africa Tech, mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo Samey Bashay alisema ni furaha kubwa kutangaza kuanzisha biashara yao katika taifa la Kenya, ambalo makampuni mengi ya kimataifa yanataja kuwa nchi ambayo iko katika eneo zuri na nafasi kubwa kibiashara.

"Leo ni siku ya kusisimua kwani tuna furaha kuleta masuluhisho ya mawasiliano ya watoa huduma wa biashara nchini Kenya. Tutaanza na huduma zetu za kiwango cha juu zaidi na kupanua utoaji wa bidhaa zetu katika miezi ijayo,” Bashay alinukuliwa na jarida hilo.

Kufikia sasa, kampuni ya mawasiliano ya Safaricom ambayo imekuwa ikitoa huduma kwa zaidi ya miaka 20 inatajwa kuongoza katika utoaji wa huduma za mawasiliano kwa asilimia kubwa huku ikifuatwa na Airtel.

Telkom ambayo haina miaka mingi katika soko la mawasiliano nchini inaibuka ya tatu katika utoaji huduma za mawasiliano Kenya.

Mwaka jana, Safaricom walipanua huduma zao za mawasiliano katika taifa jirani la Ethiopia ambapo wametaja mafanikio makubwa huku wakipata wateja wengi chini ya muda mchache ambao wamekuwa nchini Uhabeshi.