Mfuasi sugu wa Odinga achomewa nyumba yake ya msonge, MP Salasya aahidi kumjengea

Nuru aliitisha msaada akilia baada ya nyumba yake ya nyasi kuchomwa na watu wasiojulikana.

Muhtasari

• Salasya alitoa ahadi ya kumjengea nyumba nyingine huku pia akiahidi kumsaidia kurudi Nairobi baada ya kukamilika kwa shughuli hiyo.

Salasya aahidi kumjengea Okanga nyumba
Salasya aahidi kumjengea Okanga nyumba
Image: Twitter

Mbunge wa Mumias East Peter Salasya ameahidi kumjengea Nuru Okanga, mfuasi sugu wa kinara wa Azimio nyumba mpya baada ya watu wasiojulikana kuichoma nyumba yake ya msonge.

Jamaa huyo ambaye amekuwa akionekana kwenye video akimshambulia vikali rais Ruto na serikali yake huku akimtetea Odinga alitoa taarifa za kuvunja moyo kuwa wakati ako Nairobi kuhangaika na maisha, watu wasiojulikana walivamia nyumbani kwao na kutia nyumba yake ya msonge moyo.

Okanga akizungumza na blogu moja, alisema kuwa bado hajapata nauli ya kusafiri kuenda kwao Kakamega ili kujua ni nini kilitokea lakini akadokeza kuwa huenda ni wale wanaotofautiana na msimamo wake kisiasa ambao ndio walitekeleza kitendo hicho wakifikiri kuwa alikuwepo ndani au pengine mtoto wake alikuwepo ndani ili kumteketeza.

“Wale mlifikiria mngenipata ndani au mpate mtoto wangu ndani ili kumchoma, pole. Mmekuja kuchelewa. Mimi wakati napiga siasa mama yangu au familia yangu huwa haiku, mbona mnaenda kuniharibia mali yangu nyumbani? Nawaomba mtafute Okanga kibinafsi na muachane na familia yangu,” Okanga alisema.

Baada ya kulilia msaada kutoka kwa wahisani wema kumsaidia kujenga nyumba nyingine, hatimaye mbunge Salasya alikutana naye na kutoa ahadi ya kumjengea nyumba nzuri ya kisasa.

“Nuru Okanga hawakufanyia poa kukuchomea nyumba si poa lakini nitakujengea nyumba ndio urudi tena Nairobi ....wakati huo huo ilikuwa vizuri kukutana na wewe kwa mara ya kwanza. Mimi pia ni mtu wa chini na lazima nisaidie mtu wa chini kama Okanga,” Salasya alisema kwenye video aliyoipakia Twitter.