Msichana wa Gredi 6 apatikana amekatwa, kung'olewa macho na kufungwa ndani ya gunia

Macho ya msichana huyo yaling'olewa, mguu wake wa kulia ulikatwa na kuchunwa ngozi na nyeti zake zilikuwa zimeharibiwa vibaya.

Muhtasari

• Vidokezo vinaonyesha kuwa huenda alitekwa nyara na kuteswa mahali pengine kabla ya mwili wake kutupwa kwenye shamba la mahindi

Mwili wa marehemu
Mwili wa marehemu
Image: Instagram//Azam

Hali ya taaruki ilitanda katika kijiji cha Maili Tisa, Loitoktok kaunti ya Kajiado baada ya wanakijiji kupata mwili wa mtoto wa darasa la sita umekatwa katwa na kufungwa ndani ya gunia.

Kulingana na Nation, Msichana huyo wa Darasa la Sita aliripotiwa kutoweka Januari 4 na wazazi wake na hivyo kusababisha msako mkali. Shahidi alisema macho ya msichana huyo yalitolewa nje, mguu wake wa kulia ulikatwa na kuchunwa ngozi.

Kamanda wa Polisi wa Kajiado Kusini, Shadrack Ruto alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa msichana huyo pia alinajisiwa.

"Sehemu zake za siri ziliharibika sana. Bado hatujabaini sababu ya mauaji hayo lakini pia tunashuku dhabihu ya uchawi," Bw Ruto alinukuliwa na Nation.

Wakati polisi wakiweka pamoja harakati za mwisho za msichana huyo, vidokezo vinaonyesha kuwa huenda alitekwa nyara na kuteswa mahali pengine kabla ya mwili wake kutupwa kwenye shamba la mahindi.

Mwili huo ulipelekwa katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya kaunti ndogo ya Loitokitok ukisubiri kufanyiwa upasuaji.

Tukio hilo linatokea wiki kadhaa baada ya tukio sawia kuripotiwa katika kaunti ya Kisii ambapo pia mtoto mdogo alipatikana amenyofolewa macho, japo alikuwa hai.

Tangu mwaka 2023 kuanza takribani wiki mbili zilizopita, visa kadhaa vya kutia machungu moyoni vimekuwa vikiripotiwa katika kaunti mbali mbali humu nchini, wengi wakihisi huenda kuna dhabinu za uchawi au msongo wa mawazo umekumba wengi wa Wakenya kufuatia ugumu wa maisha.

Alhamisi jioni, Mwili wa mwalimu mmoja wa kiume ulipatikana katika nyumba yake ukiwa umegongelewa misumari ndani ya jeneza lenye mwonekano wa boti, wiki tatu baada ya kuripotiwa kutoweka kwa njia tata.