'Mtoto wa Mau Mau' Rigathi Gachagua aingilia kati suala la afya ya mjane wa Dedan Kimathi

Mukami Kimathi, mke wa shujaa wa Mau Mau Dedan Kimathi anazuiliwa katika hospitali moja Nairobi kwa bili ya zaidi ya milioni moja.

Muhtasari

• DP Gachagua alisema kuwa akifika Nairobi atamtembelea hospitalini na kuona njia mbadala za kumsaidia.

• Pia alimtakia afueni ya haraka huku jukumu hilo akimtwika mbunge wa Embakasi ya kati kulishughulikia kabla hajafika kutoka Bomet.

Gachagua kuingilia kati kulipa bili ya mjane wa Dedan Kimathi
Gachagua kuingilia kati kulipa bili ya mjane wa Dedan Kimathi
Image: Twitter

Naibu wa rais Rigathi Gachagua amedokeza kuwa atachukua hatua madhubuti kuhusu afya ya mke wa aliyekuwa kiongozi wa kundi la wapigaji uhuru wa Mau Mau, Dedan Kimathi, Mukami Kimathi ambaye amezuiliwa katika hospitali moja jijini Nairobi kwa kutolipa ada ya matibabu.

Kulingana na taarifa zilizopo kwa siku kadhaa sasa, Mukami amelazwa katika hospitali hiyo na bili ya matibabu imepita kiasi cha shilingi milioni moja pesa za Kenya ambapo amekuwa akiitisha msaada kutoka kwa wahisani wema ili kuruhusiwa kuenda nyumbani. 

Gachagua amedhibitisha kuwa taarifa hizo ziliwahi mfikia yeye na rais Ruto na kusikitishwa kwamba bado hajapata msaada.

“Nina huzuni kwamba Mukami, mke wa shujaa wetu, Field Marshal Dedan Kimathi Wachiuri, amekuwa mgonjwa na amelazwa katika Hospitali moja jijini Nairobi. Jambo hili lililetwa kwangu jana nikiwa katika ziara ya kikazi huko Nyanza na H.E. Rais Williams Ruto,” DP Gachagua alisema.

Inasemekana kuwa mjane huyo mkongwe amekuwa akizuiliwa katika hospitali hiyo kutokana na kutolipa bili hiyo, hata baada ya kupokea matibabu na hali yake ya afya kunawiri.

Karangu Muraya alichapisha video ya mkongwe huyo akiwa katika kitanda cha hospitali akiitisha msaada, na kuitaka serikali kuona huruma na kumlipia bili hiyo ili aruhusiwe kuondoka hospitalini.

Gachagua ambaye anakongamana na rais Ruto katika ibada ya pamoja kaunti ya Bomet baada ya kumalizika kwa ziara ya Nyanza alisema kuwa ameshangaa sana kuwa mama Mukami bado amezuiliwa hospitalini.

Alisema kuwa amemtwika jukumu la kuangalia suala hilo mbunge wa Embakasi ya Kati huku akidokeza kuwa pindi atakaporejea Nairobi atamtembelea na kuona jinsi ya kutoa msaada wake.

“Katika hili, nimempa kazi Mbunge wa Embakasi ya Kati Mhe. Benjamin Gathiru a.k.a Meja Donk kuangalia hali yake kwa haraka. Nikirudi Nairobi baadaye leo, nitapata muda wa kumtembelea mama yetu ili kuangalia maendeleo yake na kutathmini afua zinazowezekana kufanya maisha yake kuwa ya starehe zaidi. Namtakia apone haraka na baraka za Mungu.”

Gachagua amekuwa akinukuliwa akijipiga kifua kuwa wazazi wake walikuwa wanachama wa kundi la Mau Mau.