Mwanamume mshukiwa wa wizi akamatwa na nguo za wanawake ndani ya gari lake

Ndani ya gari hilo, kulipatikana silaha ghafi, nguo za wanawake, simu kadhaa miongoni mwa vitu vingine.

Muhtasari

• Polisi walisema kuwa wezi hao walikuwa wametoka Nairobi na kuenda kufanya uhalifu katika kaunti za Nyandarua na Laikipia.

• Nguo za wanawake zilishukiwa kuwa za waathirika kwa ujambazi kutoka kwa wenye gari hilo.

Mwanamume mshukiwa wa ujambazi aliyekamatwa na nguo za kike
Mwanamume mshukiwa wa ujambazi aliyekamatwa na nguo za kike
Image: Facebook//DCI

Mwanamume mmoja alitiwa mbaroni na makachero wa DCI katika kaunti ya Nyandarua baada ya gari lake kushukiwa kuwa la ujambazi.

Kulingana na ripoti iliyochapishwa na DCI, maafisa wa polisi walikuwa wakishika doria katika mji wa Nyahururu ambapo walikuta gari hilo ambalo ndani yake waliona lina nambari tofauti za usajili zilizokuwa zimewekwa katika kioo cha mbele.

Hapo ndipo walilishuku na kulisimamisha ambapo ndani mwake walimpata mwanamume huyo pamoja na silaha zingine hatari.

“Baada ya kufanya upekuzi wa kina ndani ya gari hilo aina ya Toyota Noah, majasusi hao waliokuwa na pua ya kunusa ugaidi walipata silaha ghafi, simu sita za mkononi, bidhaa mbalimbali zikiwa kwenye begi la bunduki na nguo za wanawake wanaoaminika kuwa wahanga wa wizi. Wakati wapelelezi waliokuwa katika kitengo cha usaidizi wa operesheni walipolinganisha maelezo na wenzao wa DCI Laikipia, iligundulika kuwa gari hilo lilikuwa kwenye rada yao baada ya kuhusika katika matukio mbalimbali ya wizi,” sehemu ya taarifa ya DCI ilisoma.

Kando na silaha ghafi, pia nguo za wanawake zilipatikana ndani ya gari hilo, zikishukiwa kuwa za waathiriwa wa wizi kutoka kwa majambazi hao wenye gari.

Kufikia sasa, walalamishi 4 tayari wamejitokeza na kumtambua mshukiwa aliyekamatwa kwa jina William Mwangi, ambaye alifichua kuwa yeye na washirika wake ambao bado walikuwa mbioni, walikuwa wamesafiri kutoka Nairobi kutekeleza wizi katika maeneo hayo.

Mshukiwa huyo kwa sasa yuko katika kituo cha polisi cha OlKalou akishughulikiwa ili afikishwe mahakamani, huku maafisa wa upelelezi wakizidisha msako wa kuwatafuta washirika wake ambao wanatoroka kwa sasa.