Simba Arati: Nilipata shilingi 250K yangu ya kwanza nikiwa Nairobi kupitia kwa Rachel Ruto

"Nimemjua mama wa taifa ambaye ni mke wa rais akiwa anafanya biashara ya usafiri katika ofisi yake." - Arati alisema.

Muhtasari

• Gavana huyo wa Kisii alielezea kuwa Rachel ndiye alimwekea saini ya kukubaliwa kuingia katika biashara yake ya kwanza kama wakala wa usafiri.

• Alimshukuru kwa baraka hiyo ambayo ilimpa faida na kupata elfu 250 zake za kwanza.

Arati azungumza jinsi Rachel Ruto alimsaidia Nairobi
Arati azungumza jinsi Rachel Ruto alimsaidia Nairobi
Image: Facebook

Gavana wa Kisii, Simba Arati amefunguka makubwa jinsi mama wa taifa Rachel Ruto alimsaidia enzi akianza kuchakarika kutafuta riziki katika kaunti ya Nairobi.

Ruto alikuwa akizungumza katika ibada ya kanisa ambayo Mama Rachel alihudhuria kwenye kaunti hiyo ya Kisii ambapo alisema kitu ambacho wengi hawajawahi jua kwa miaka mingi kuwa yeye na mama Rachel ni marafiki ambao wametoana mbali sana hata kabla gavana huyo hajaanza safari yake ya siasa.

Arati alisema kuwa Rachel ndiye alimsaidia elfu 250 ya kwanza katika kaunti ya Nairobi kuanzia biashara yake.

“Nataka nielezee kitu kimoja, nimemjua mama wa taifa ambaye ni mke wa rais akiwa anafanya biashara ya usafiri katika ofisi yake. Mtu aliyefanya nikapata shilingi elfu 250 za kwanza nikiwa Nairobi ni huyu mama,” Arati alisema.

Alisema kuwa wengi walikuwa wanajua alikuwa anauza mboga ambazo zilimsaidia kujichanga katika suala la karo ya chuoni.

“Najua watu wengi wanajua nilikuwa nauza mboga, nikaenda chuo, nikamaliza nikarudi na kuendelea kuuza mboga nikashindwa sasa nifanye nini, ndio nikaingia katika biasharakama wakala wa usafiri, na ningeitaji mtu wa kuniwekea saini ili kufaulu. Nikaenda nikampata kwa ofisi yake na hakuwa ananijua, akaniwekea kidole. Nikafanya biashara ya kwanza ambayo ilikuwa ni Baraka kutoka kwa mama huyu,” Arati alisema huku akimshukuru mama Rachel.

Licha ya Arati kuwa katika mrengo wa Azimio ambao alishinda nao ugavana, alisema hakuwa na ubaya wowote na chama cha UDA ambacho kinaongozwa na rais Ruto, kwani anajua jinsi mama Rachel alimpa Baraka ya biashara ya kwanza ambayo ilimfungulia mfululizo wa faida mpaka kuwa mtu tajika na hatimaye kujitosa kwenye siasa alikowania ubunge Dagoretti North.