Mashabiki wa Arsenal waliozuiliwa Uganda waachiliwa huru

Polisi walisema hawakuwa na kibali cha kufanya maandamano hayo ambayo ni kosa kisheria.

Muhtasari

•Walikuwa wamevalia jezi nyekundu ya klabu hiyo na kubeba kombe la mfano wakati walipokamatwa Jumatatu.

•Mmoja wa mashabiki hao aliwaambia waandishi wa habari kwamba "wangeomba ruhusa ya kusherehekea ikiwa Arsenal itashinda ligi kuu".

Image: BBC

Mashabiki wanane wa Arsenal waliokamatwa katika jiji la Jinja nchini Uganda baada ya kusherehekea ushindi wa klabu hiyo dhidi ya Manchester United katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza wameachiliwa huru.

Walikuwa wamevalia jezi nyekundu ya klabu hiyo na kubeba kombe la mfano wakati walipokamatwa Jumatatu.

Polisi walisema hawakuwa na kibali cha kufanya maandamano hayo ambayo ni kosa kisheria.

Lakini siku ya Jumanne kikosi cha usalama kilikubali kuwaachia huru na kuwapa onyo, alisema James Mubi, msemaji wa polisi wa eneo hilo.

Mmoja wa mashabiki hao aliwaambia waandishi wa habari kwamba "wangeomba ruhusa ya kusherehekea ikiwa Arsenal itashinda ligi kuu".

"Tutasheherekea katika uwanja wa Bugembe," aliyejitangaza kuwa balozi wa Arsenal nchini Uganda aliongeza.

Msemaji huyo wa polisi alidai kuwa mashabiki hawakujua mambo ya msingi kuhusu klabu hiyo kwamba ni mwaka gani ambao Arsenal ilicheza bila kushindwa mchezo wowote na walimtaja mlinda mlango wa zamani wa Uganda kuwa mchezaji wa Arsenal.