Kijana mwenye digrii 2 bila kazi kwa miaka 9 hatimaye apata kazi kwa gavana Mwangaza

Kijana huyo alionekana na bango mgongoni akiomba msaada wa kazi.

Muhtasari

• Mwangaza alitoa wito kwa viongozi wote kufanya mazingira ya kupata kazi kwa vijana wenye elimu na tajriba kuwa rahisi ili kuwakimu kimaisha.

Makamba akiwa ofisini mwa gavana Mwangaza
Makamba akiwa ofisini mwa gavana Mwangaza
Image: Facebook

Mwanamume mmoja kutoka kaunti ya Meru ambaye picha yake akiwa ameshikilia bango zilienezwa wiki siku kadhaa zilizopita hatimaywe amepata faraja kupitia mkono wa gavana Kawira Mwangaza.

Mwanamume huyo alikuwa na bango ambalo lilikuwa linatoa maelezo yake akisema ana shahada mbili lakini hajawahi pata kazi. Alikuwa anaomba msaada wa kupata kazi.

Ombi lake lilimfikia gavana Mwangaza ambaye ameangaza nuru usoni mwake kwa kumpa kazi.

“Kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la Meme Samuel Makamba ambaye picha yake ilisambaa ikimuonyesha akitafuta kazi mtaani huku akiwa amebeba bango kwenye mgongo wake lenye maombi na maandishi ya manila, hatimaye anaweza kuwa na uhakika wa usalama wa ajira,” gavana Mwangaza alisema.

Licha ya Samuel kuwa na Shahada 2 za Shahada na cheti cha CPA, amekuwa akitafuta kazi yenye faida bila mafanikio kwa miaka 9 iliyopita. Nimekutana naye leo na kumuahidi kumpa kazi, gavana huyo ambaye alinusurika kung’atuliwa madarakani alisimulia.

Mwangaza alitoa wito kwa viongozi wote kufanya mazingira ya kupata kazi kwa vijana wenye elimu na tajriba kuwa rahisi ili kuwakimu kimaisha.

“Kama viongozi, ni lazima tuangalie ustawi wa vijana wetu na kuwatengenezea fursa za kuwaingizia kipato tunapojitahidi kupunguza kasi ya ukosefu wa ajira nchini mwetu.”

Hata hivyo, gavana Mwangaza hakuweka wazi ni kazi gani atampa kijana huyo.

Gavana huyo alinusurika mara mbili kufukuzwa madarakani baada ya madiwani wa kaunti hiyo kuanzisha mswada wa kumng’atua mamlakani, wa kwanza ukatupiliwa mbali na mahakama huku wa pili ukifika hadi bunge la seneti mbele ya jopo lililokuwa likiongozwa na seneta wa Kakamega, Boni Khalwale.

Jopo hilo liliutupilia mbali mswada huo wa MCAs wa Meru kwa kusema kuwa malalamishi yao hayakuwa na uzito wa kumfanya gavana kutimuliwa.