Kubali nilikushinda, toka ikulu Baba aingie, Wakenya walinichagua - Raila amwamia Ruto

"Tunasema ukweli, hatutaki vita, na wala hatutaki vitisho." -Odinga alisema.

Muhtasari

• "Wakenya wanastahili kiongozi waliyemchagua,” alisema.

Odinga amtaka Ruto kumuachia Ikulu
Odinga amtaka Ruto kumuachia Ikulu
Image: Facebook

Kiongozi wa muungano wa Azimio la Umoja Raila Odinga amemtaka Rais William Ruto kukubali kwamba hakushinda uchaguzi wa urais wa Agosti 2022 na kumuondokea ikuluni ili yeye aingie kule kama rais wa Wakenya.

Akiwahutubia wafuasi wake katika Kanisa la Jesus Teaching Ministry huko Donholm, Nairobi Jumapili, Raila alimkashifu vikali rais Ruto kwa kutoza ushuru mwingi nchini, huku akisisitiza kuwa hawezi hata sekunde moja kumkubali kama rais aliyeteuliwa kihalali.

“Kubali kuwa ulishindwa kwenye uchaguzi, toka Ikulu ili Baba aingie, tunasema ukweli, hatutaki vita, na wala hatutaki vitisho. Tuna haki zetu kama Wakenya, na haiwezi kuporwa na mwewe, Wakenya wanastahili kiongozi waliyemchagua,” alisema.

Odinga anatarajiwa Jumapili kuwahutubia maelfu ya wafuasi wake ambao wamefurika katika uwanja mdogo wa Jacaranda katika eneo bunge la Embakasi East jijini Nairobi ambapo atatoa muelekeo zaidi kufuatia matamshi yake kuwa hawezi kutambua ofisi hata moja inayoshikiliwa na uongozi wa Kenya Kwanza.

Ikumbukwe awali tuliripoti kuwa tayari mkuu wa DCI Mohammed Amin alishatoa taarifa kuwa kitengo hicho cha upelelezi kimejitosa katika kuchunguza madai yake kuwa kura za Agosti mwaka jana zilihitilafiwa.

Amin alisema kuwa kitengo hicho kitafanya uchunguzi wa kina na wa ndani kwani madai ya Odinga ni mazito na ambayo hajafai kuchukuliwa kwa wepesi wa kimzaha.

Aidha akizungumza katika ibada hiyo ya kanisa, Odinga alisema kuwa njia pekee ya ukweli kupatikana ni kupitia DCI kufanya uchunguzi bali ni iwapo Azimio wataruhusiwa kupitia na kufanya uchanganuzi wao wenyewe wa matokeo ambayo IEBC ilitumika kumtangaza Ruto kama rais.