Binti wa rais, Charlene Ruto asimulia jinsi hedhi ilimuabishia akiwa chuoni

Charlene alisema wlaikuwa chuoni wakati wa ibada ya kanisa wakati hedhi yake ilibisha ghafla.

Muhtasari

• Alisema hata hivi majuzi pia tukio kama hilo lilimtokea na kumpa wakati mgumu sana mbele ya rafiki zake wa kiume.

Charlene Ruto
Charlene Ruto
Image: Twitter

Binti wa taifa Charlene Ruto kwa mara ya kwanza amezungumzia aibu aliyowahi kupata wakati mmoja hedhi yake ilipokuja bila kutarajia.

Ruto ambaye alikuwa anazungumza katika chuo kikuu cha Cooperative katika mpango wake wa kusukuma utoaji wa sodo na vifaa vingine kwa watoto wa kike, alihadithia jinsi watoto wa kike wanajipata kwenye aibu siku zao za mwezi zinapobisha pasi na kutarajia kwao.

“Wakati nipo chuo cha Daystar tulikuwa na ibada ya kanisa na nilikuwa nimeketi kando na rafiki yangu mmoja. Wakati ibada iliisha tulisimama kwa maombi ya mwisho, nilipogeuka kuangalia kwa kiti changu niligundua hedhi yangu imekuja bila kutarajia. Niliaibika na kuketi chini ghafla, rafiki yangu aliniuliza nini mbaya nikamuelezea,” Binti Ruto alisema.

Charlene alisema tukio hilo lilimtokea akiwa na mri wa miaka 21. Pia alisema hivi majuzi tukio sawia lilimtokea akiwa na marafiki wake wa kiume na ulikuwa wakati mgumu sana kwake.

Binti huyo alisema kwamba mpango wake wa kuanzisha utoaji wa sodo na elimu kuhusu usafi wakati wa hedhi kwa watoto wa kike uliasisiwa baada ya kuulizia mashabiki wake mitandaoni kuhusu kile walichotaka azingatie Zaidi.

“Ni sharti tuzingatie kuzungumzia suala la afya ya siku za hedhi kwa uwazi pasi na kuficha. Hili litahakikisha kwamba tunafutilia mbali dhana potofu kuhusu hedhi kwa wanawake, kwa sababu siku za hedhi ni kitu cha kawaidac ambacho kinatokea kwa kila mwanamke,” alisema.