"Vile inasemekana, aliwekewa sumu," Babake msanii Ilagosa asema kwa majonzi

Taarifa za msano huyo wa kibao cha "Sala Zangu" ziliwekwa wazi Ijumaa wiki jana.

Muhtasari

• “Huwezi jua kuwa unaenda kufa. Unatembea na mtu kumbe yeye ni adui yako" - babake Ilagosa.

Babake Ilagosa akizungumzia kiini ha kifo cha mwanawe.
Babake Ilagosa akizungumzia kiini ha kifo cha mwanawe.
Image: Screengrab

Babake marehemu msanii wa injili Ilagosa wa Ilagosa amezungumza kuhusu madai yanayopiga misele kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kifo cha mwanawe.

Katika mahojiano na wanahabari katika ibada ya Wafu ya Ilagosa iliyofanyika Alhamisi, mzee huyo alisema kuwa ni kweli huenda mwanawe aliwekewa sumu kwenye chakula na rafiki wake wa karibu.

Alisema Ilagosa ni mtoto wake wa tano aliyemzaa miaka 40 iliyopita, mazishi yake yatafanyika Alhamisi wiki kesho nyumbani kwao kaunti ya Vihiga.

“Kwa ufupi ingawa sikuwa karibu lakini kufuatia maneno ya watu, inasemekana alipewa sumu kutoka kwa safari mahali walikuwa na ikaja ikamuathiri,” alisema mzee huyo aliyejawa majonzi na simanzi.

Pia alitoa ushauri kwa vijana haswa walioko kwenye Sanaa kuwa macho na marafiki zao wa karibu ambao huenda ndio watakuwa chanzo cha kukatisha maisha yao ghafla.

“Huwezi jua kuwa unaenda kufa. Unatembea na mtu kumbe yeye ni adui yako, ukiangalia mambo ya Ilagosa ni kama ya kirafiki tu, alifanyiwa njama na rafiki, mtu ambaye walikuwa na ukaribu naye,” Mzee huyo alishauri.

Ilagosa alifariki Ijumaa wiki jana, taarifa ambazo ziligonga vichwa vya habari kuwa alifariki kutokana na kula sumu.

Msanii mwenzake Harry Richie aliyepata umaarufu kwa jina la wimbo wa Vaida pia alizungumzia suala hilo akisema kuna uwezekano mkubwa kuwa alikula sumu ambayo alitiliwa kwenye chakula na marafiki zake wa injili.

Richie alisema walikuwa wanatarajia kufanya collabo na Ilagosa lakini ndio hivyo tena, yaliyotokea yakatokea.