Barbara Magoha: Nilihakikisha mume wangu anakula chakula changu kwa miaka 40 ndoani

"Sikuwahi muangusha, hata kama nimeshikika na shughuli nje ya nchi, nilihakikisha anakula chakula nilichokipika mimi," - Barbara.

Muhtasari

• Mimi huwa nimeshikika sana nah ii kazi yetu ya Udaktari lakini nilihakikisha anakula chakula changu - Barbara Magoha.

Mkewe Magoha asema mumewe alimjia ndotoni baada ya kufa
Mkewe Magoha asema mumewe alimjia ndotoni baada ya kufa
Image: Maktaba, Screengrab

Mjane wa profesa Magoha, Barbara Odudu amezungumza kitu ambacho kinampa faraja hata baada ya kifo cha mume wake.

Katika hafla ya kumpa buriani za mwisho Profesa George Magoha, Barbara alisema kuwa mumewe aliyefariki akiwa na Zaidi ya miaka 70 alifariki akiwa ameishi maisha ambayo angeyataja kama kamilifu naye muda wote.

Barbara alisema kuwa kitu kimoja anachojivunia kumfanyia mumewe katika muda wote wa miaka 43 ya ndoa yao ni kumpikia kila mara.

Aliwashangaza waombolezaji alipofichua kuwa katika muda huo wote wa miaka 43, Magoha hakuwahi kula chakula kilichopikwa na mtu mwingine akiwa nyumbani kwao isipokuwa chakula ambacho kimepitia mikononi mwa upishi wake kama mke wake – jambo ambalo alilivuta nyuma kwenda kwa tamaduni za kufundwa kama mwanamke wa jamii ya Calabar nchini Nigeria.

Daktari Barbara alisema kuwa kazi yake kama daktari si rahisi hivyo lakini alihakikisha kuwa hata wakati ameshikika sana na shughuli rasmi nje ya nchi, bado alihakikisha mumewe anakula chakula alichokipika yeye!

“Ninafarijika kwamba mume wangu anaenda baada ya kuishi na mimi kwenye ndoa kwa miaka 40. Katika muda huo wote, nilimpikia chakula na alikila chakula changu mimi tu. Mimi huwa nimeshikika sana nah ii kazi yetu ya Udaktari lakini nilihakikisha anakula chakula changu. Sikuweza kumuangusha hata mara moja, mimi ni mwanamke wa jamii ya Calabar,” Barbara alisema.

Juzi katika ibada ya wafu iliyofanyika Nairobi katika kanisa la Consolata Shrine, Barbara alisema kuwa alifundwa enzi za usichana wake jinsi ya kumdekeza na kumhendo mwanamume na ndio maana ndoa yao ilidumu kwa Zaidi ya miongo minne.

Alifunguka kuwa licha ya watu wengi kudhani ndoa yao ilikuwa kamilifu, hali haikuwa hivyo kani changamoto ni sehemu ya ndoa yoyote ile, kikubwa alichokitaja ni kuvumiliana wakati mwenzako yuko chini, unamuinua huku akifutilia mbali uwezekano wa ndoa kuwa na mchango wa 50-50 kutoka pande zote.

Alisema suala la 50-50 si lazima kwani kuna wakati mmoja ako asilimia 60 mwenzake akiwa 40%, Wakati mwingine mmoja yuko sawa kwa asilimia 80 na mwenzake akiwa 20, kikubwa bora mnafikisha 100%.