Ezekiel Mutua azungumzia mazingira ya kifo cha mama yake, "Hakuwa mgonjwa!"

“Aliamka asubuhi jana akiwa salama na mzima wa afya, akanywa kiamsha kinywa na kuketi chini kwenye veranda akapumzika."

Muhtasari

• Hivi majuzi, walikuwa naye na alikumbuka kuwa kwa jinsi walifurahia, huenda Mungu alikuwa anawataarifa kuwa muda wake umekaribia.

Mutua azungumza nyakati za mwisho walipokuwa na mama yake.
Mutua azungumza nyakati za mwisho walipokuwa na mama yake.
Image: Facebook

Jumanne Februari 14, mkurugenzi mkuu wa bodi ya kutetea hakimiliki za wasanii humu nchini MCSK, Dkt Ezekiel Mutua alitangaza kufiwa na mama yake.

Mutua sasa amefunguka kwa upana kiini cha kifo cha mama yake, akipakia picha za mwisho wakifurahia naye nje ya nyumba yake kwenye kivuli.

Mutua alisema kwamba mama yake hakuwa mgonjwa. “Aliamka asubuhi jana akiwa salama na mzima wa afya, akanywa kiamsha kinywa na kuketi chini kwenye veranda akapumzika kwa Amani katika kiti chake pale pale alikokuwa anapenda kuketi nje ya nyumba yake.”

Mkurugenzi huyo wa MCSK alisema kwamba hakuna kitu kilichowaandaa kwa kifo cha mama yao kwani hakuonesha dalili yoyote ya kuumwa.

Picha alizopakia wakiwa naye ndizo za mara ya mwisho hivi majuzi akiwa nyumbani pamoja na ndugu yake wakimshika mikono kwa tabasamu kubwa kwenye nyuso zao.

“Hizi ndizo picha za mwisho tukijumuika na mama juzi tu. Alikuwa mwingi wa furaha na alituchekesha kwa mizaha ya utani na tulishiriki chakula pamoja,” Mutua alikumbuka.

Alihisi kwamba kwa jinsi walikuwa wanamshika mama yao mikono yeye na ndugu yake, ilikuwa kama igizo la kumpungia buriani bila wao kujua kwamba Mungu alikuwa anawatumia ujumbe wa kufurahia naye mara ya mwisho kabla ya kumpumzisha.

“Ninatazama picha hizi na kugundua kuwa wakati fulani mimi na kaka yangu mkubwa tulikuwa tumemshika mkono bila hiari katika mazungumzo ya uhuishaji. Kwa kutazama nyuma, nadhani Mungu alikuwa akitutayarisha kwa ajili ya kuondoka kwake, lakini hatukutambua. Sasa nyakati hizi zina maana ya kweli. Nenda vizuri mama. . .” Mutua aliomboleza kwa maandishi yenye hisia za uchungu.

Alitarajiwa kuhudhuria kongamano la wanaume maarufu ‘Men’s Conference’ lililofanyika Februari 14 katika ukumbi wa Carnivore jijini Nairobi lakini hilo halikuwezekana kwani saa chache kabla ya kuanza mkutano, aliwataarifa mashabiki na wafuasi wake mitandaoni tanzia ya kifo cha mama yake.

Mutua ametoa shukrani kwa wafuasi wake mitandaoni kumfariji kipindi hiki anaomboleza.