Mwanafunzi afariki kwa kuchapwa na mwalimu wiki 2 tu baada ya kujiunga kidato 1

Kiptanui mwenye umri wa miaka 16 alijiunga shuleni wiki 2 zilizopita kwa kuchelewa kutokana na karo.

Muhtasari

• Inaarifiwa alipigwa na mwalimu baada ya kuibia jibu kutoka kwa kitabu wakati wa somo la Fisikia Ijumaa mchana.

crime scene
crime scene

Mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya upili ya Chemase ameripotiwa kufariki kutokana na kile kilitajwa kuwa ni kushambuliwa kwa viboko na walimu wa shule hiyo.

Kelvin Kiptanui mwenye umri wa miaka 16 alifariki alipokuwa akipokea matibabu katika hospitali ya Nandi Level Four baada ya kukimbizwa hapo kufuatia kipigo hicho.

Kulingana na ripoti iliyopeperushwa kwenye kituo kimoja cha runinga humu nchini, polisi katika eneo la Tinderet tayari wameanzisha uchunguzi kubaini mazingira ambayo mwanafunzi huyo alifariki kufuatia madai kwamba alichapwa na walimu.

Katika taarifa ya awali, Kiptanui alichapwa na mwalimu wake baada ya kubukua kitabu ili kujibu swali alilokuwa ameulizwa na mwalimu wa somo la Fisikia Ijumaa alasiri.

Kiptanui alikuwa amesajiliwa kama mwanafunzi wa shule hiyo takribani wiki mbili zilizopita.

Kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Tinderet Ali Jire alisema kisa hicho kiliripotiwa Jumapili na mamake marehemu.

"Ni tukio tata sana kwa sababu shule bado haijatoa ripoti rasmi kwa polisi kuhusu kifo hicho na mazingira yanayozunguka kifo," Jire alisema.

“Marehemu aliripoti sekondari ya Chemase wiki mbili zilizopita. Alichelewa kuripoti kutokana na ukosefu wa ada. Mwili wa marehemu ulihamishiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya Nandi-Hills ukisubiri uchunguzi wa uchunguzi kubaini chanzo cha kifo hicho,” sehemu ya ripoti hiyo ilisema.

Itakumbukwa adhabu ya viboko shuleni ilibatilishwa miaka michache iliyopita baada ya kubainika kwamba walimu walikuwa wanaitumia visivyo na kuwajeruhi wanafunzi badala ya kuwatoa makosa.

Aliyekuwa waziri wa elimu hayati George Magoha alikashifu vikali vitendo vya walimu kuwashambulia watoto kwa vibojko shuleni huku akitoa wito kwa tume ya kuajiri walimu TSC kuwachukulia hatua kali za kisheria walimu ambao wanapatikana wakiwachapa wanafunzi viboko shuleni.