Mwanamume aliyemnajisi binti yake akamatwa akimtafutia huduma ya kutoa hiyo mimba

Msichana huyo wa miaka 18 alikiri kuwa babake amekuwa akimlazimisha kushiriki mapenzi naye kwa miaka 4. Alikuwa na mimba ya babake ya miezi 3.

Muhtasari

• Msichana huyo anasemekana kuwa na ujauzito wa miezi mitatu.

• Kulingana na taarifa, Mwanamume huyo anadaiwa kuhusika na ujauzito huo.

Mwanaume aliyekamatwa
Mwanaume aliyekamatwa
Image: Sagwe

Baba wa watoto wanne mwenye umri wa miaka 39 anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Njoro kaunti ya Nakuru baada ya kukamatwa akijaribu kumtoa mimba bintiye mwenye umri wa miaka 18.

Kulingana na taarifa, Mwanamume huyo anadaiwa kuhusika na ujauzito huo.

Chifu msaidizi wa lokesheni ndogo ya Amani Milka Lang'at alisema kuwa mwanamume huyo alikuwa ameenda kumchukua bintiye shuleni Kitale, Kaunti ya Trans Nzoia kwa lengo la kumtoa mimba.

Msichana huyo anasemekana kuwa na ujauzito wa miezi mitatu.

Mwanamume huyo anasemekana kulaghaiwa na wanakijiji kusafiri kurudi nyumbani kutekeleza utaratibu huo kabla ya kuongozwa hadi mtaa wa nyuma katika mji wa Njoro.

Langat alisema kuwa msichana huyo alikiri kulazimishwa kufanya mapenzi haramu na babake kwa miaka minne na kusema alipojaribu kumtaka mamake kuingilia kati, alionywa kuhusu madhara mabaya.

Alisema mwanamume huyo atafunguliwa mashtaka ya kujamiiana na unajisi miongoni mwa mashtaka mengine polisi watakapokamilisha uchunguzi wao.

“Leo tulikwenda kuwatembelea nyumbani kwao na kuzungumza na mke kuhusu kilichokuwa kikitokea ili aeleze ni kwa nini amekuwa kimya na iwapo mabinti wengine wamekuwa wakipitia hali hiyo,” alisema.

Visa vya wazazi wa kiume kuwadhulumu mabinti zao kimapenzi vimekithiri nchini huku wazazi wa kike wakitakiwa kuwa macho Zaidi ya kuripoti wanaume hao fisi ambao hunyemelea mabinti zao.

Pia serikali imewataka machifu kutosuluhisha visa kama hivyo kwa njia za kinyumbani na badala yake kupiga ripoti kwa taasisi husika.