Babu Owino:Kumkamata Baba kutasababisha uharibifu wa nchi hii

Amesema iwapo polisi watajaribu kumkamata kiongozi huyo wa upinzani basi wafuasi sugu wa Raila watamuokoa

Muhtasari
  • Wabunge wa UDA walitaka chama cha Azimio wawajibikie hasara na uharibifu uliokadiriwa wakati wa maandamano Jumatatu.
Mbunge wa Embakasi East Babu Owino
Image: Facebook// Babu Owino

Mbunge wa  Embakasi mashariki na mfuasi sugu wa ODM Paul Ongili almaarufu Babu Owino amewasuta viongozi wa chama cha UDA kwa kutoa wito kwa polisi kuwakamata rais wa zamani Uhuru Kenyatta na Raila Odinga.

Akitumia ukurasa wake wa Twitter muda mfupi baada ya wanachama wa UDA kuwahutubia wanahabari, Babu amedai kuwa Raila Odinga ni chombo cha nne cha serikali pamoja na mahakama, bunge na utendaji.

Amesema iwapo polisi watajaribu kumkamata kiongozi huyo wa upinzani basi wafuasi sugu wa Raila watamuokoa na hii itasababisha uharibifu mkubwa kwa nchi ambayo hakuna mtu anataka kuona.

"Tuna mikono 4 ya serikali;1.Raila Amolo Odinga 2.Bunge 3.Mtendaji 4.MahakamaKuweka nia ya kumkamata Baba kutasababisha uharibifu wa nchi hii, na tuko tayari kuanza upya,"Alisema Babu Owino

Wabunge wa UDA walitaka chama cha Azimio wawajibikie hasara na uharibifu uliokadiriwa wakati wa maandamano Jumatatu.

Maandamano hayo yalisababisha kifo cha mwanafunzi wa chuo kikuu cha Maseno.

Katika taarifa yake siku ya Jumanne, Kenya Kwanza ilieleza kuwa maandamano yaliyoongozwa na kiongozi wa Azimio Raila Odinga yalifikia kilele kwa "uvamizi wa uporaji, uharibifu usio na akili, kuendesha vita na maafisa wa kutekeleza sheria", tofauti na yale yaliyokuwa yameahidiwa kuwa maandamano ya amani.

"Maandamano ya Bw. Odinga yaliyoitwa ya amani yalikuwa kampeni ya uwazi ya ujambazi mkubwa wa mijini na sio kitu kingine chochote."