Kisii: Gavana afuta wahudumu wa mochwari kwa 'kucheza na maiti'

Arati alisema alitoa agizo kwa daktari mkuu kuwaondoa wawili hao mara moja kwenye orodha ya wafanyikazi wa mochwari hiyo.

Muhtasari

• "Nimetoa agizo kwa daktari hawa watu waende nyumbani sasa hivi tu, hakuna kazi nyingine,” Arati alisema.

Gavana wa kaunti ya Kisii
Gavana wa kaunti ya Kisii
Image: Facebook

Gavana wa kaunti ya Kisii Simba Arati amezuru chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya rufaa ya Kisii ambapo siku chache zilizopita kililalamikiwa kwa kutekeleza maiti.

Familia moja iliyokuwa imekwenda kuchukua mwili wa mpendwa wao ililalamika baada ya kupata maiti ikiwa katika hali duni ambapo walisema kuwa ilikuwa imedokolewa na panya.

Gavana huyo baada ya kufika katika makafani hiyo, alitoa hakikisho kwamba tayari uongozi wake umechukua hatua ya haraka kwa kuwasimamisha kazi wahudumu wawili wa mochwari hiyo kwa utepetevu kazini.

Pia gavana Arati alisema kuwa alipokea malalamishi mengi kuwa wahudumu hao walikuwa wanatoza watu pesa ili kuhudumia miili na wale waliokuwa wakikataa kutoa kiasi cha pesa mwili wa mpendwa wao uliuwa unatelekezwa katika hali duni kwenye chumba hicho cha kuhifadhi maiti.

“Kitu ambacho nimefanya ni kwamba wale wahudumu wawili wa mochwari nimewatuma nyumbani leo. Kwa sababu watu hawa walikuwa wanatoza pesa ili kuosha miili. Ni ufisadi tu. Unaweza tafakari kwamba watu hawa walikuwa wanapata pesa kwa wafu hapa. Nimetoa agizo kwa daktari hawa watu waende nyumbani sasa hivi tu, hakuna kazi nyingine,” Arati alisema.

Gavana huyo alisema tayari wameshafanya mpango na kuwaleta wahudumu mashuhuri wa mochwari kutoka hospitali moja nchini ambayo hata hivyo hakuitaja kwa jina akisema wao ndio watakuwa wanashughulikia maiti kwa njia inayofaa.