KOT: Seneta wa Nandi kikaangoni kwa kudai ng'ombe wa Ruto alizaa ndama 3 mapacha

Wengine walihisi Cherargei alitumia mfano wa ng'ombe mwenye mapacha 3 kuashiria Ruto atabadili katiba na kuwania muhula wa tatu.

Muhtasari

• KOT walimtumbua baada ya kuibua ukweli kwamba ng'ombe huyo ni wa Mjerumani aliyezaa mapacha 3 na wala si wa Ruto huku Kenya.

• Lakini wengine walihisi ujumbe wake Cherargei ulikuwa kiashiria kwamba Ruto huenda akataka kuwania muhula wa tatu kama rais.

Seneta wa Nandi adai ng'ombe wa Ruto alizaa mapacha 3.
Seneta wa Nandi adai ng'ombe wa Ruto alizaa mapacha 3.
Image: Twitter

Seneta wa Nandi, Samson Cherargei amejipata kwenye kikaango kilali cha watumizi wa Twitter baada ya kudai kwamba ng’ombe wa rais William Ruto alizaa ndama watatu mapacha.

Bw Cheragei mnamo Aprili 11, 2023, alinaswa katika kile wanatwitter walisema ni uwongo alipochapisha sasisho kwenye mitandao ya kijamii kuhusu mali kubwa inayomilikiwa na Rais William Samoei Ruto.

Mwanasiasa huyo muongeaji na mara nyingi mwenye utata, alidai kuwa ng’ombe mmoja wa Rais Ruto alizaa ndama watatu kimuujiza na kuwatumia kama ishara ya uongozi wa Rais.

“Ng’ombe wa H.E Ruto amezaa mapacha watatu wa uongozi wake wa mfano. Miaka 5 ya kurudisha nyuma shimo la deni lililoundwa na Uhuru + Raila katika mageuzi ya kiuchumi. Miaka 5 kwa utulivu wa kiuchumi. Miaka 5 ya Kenya ustawi wa maziwa + asali miaka 15 ya mabadiliko ya kiuchumi bila kukatizwa,” alisema Seneta Cherargei.

Hata hivyo, kauli yake ilionekana kuibua utata mwingi, baadhi wakimsuta kwa kudanganya kuwa ng’ombe wa Ruto amezaa mapacha 3 na wengine wakihisi seneta huyo alikuwa anaashiria kuwa Ruto atawania mihula mitatu, kinyume na ukomo wa mihula miwili kwa rais kama inavyofafanuliwa katika katiba ya Kenya mwaka 2010.

Hata hivyo, wadadisi wa Twitter walizama Zaidi na kuibua picha halisi za mwenye ng’ombe huyo aliyezaa mapacha 3.

Ng’ombe huyo anamilikiwa na wazungu nchini Ujerumani.

Lakini swali ambalo limesalia kwenye vichwa vya wengi ni Je, Seneta wa Nandi Samson Cherargei alidanganya kuhusu ng'ombe wa Rais William Ruto kuzaa mapacha watatu au tweet yake ilikuwa ujumbe wa kificho kupendekeza kwamba Mkuu wa Nchi atafikiria kubadilisha katiba ili kuwania muhula wa tatu?