Kirinyaga: Muuza bangi ajisalimisha, aandika barua ya kuomba msamaha

Mwanamume huyo alijisalimisha baada ya mbunge wa Kirinyaga ya kati kumuanika wiki mbili zilizopita.

Muhtasari

• Pia aliwasilisha barua hiyo kwa naibu kamishna wa Kirinyaga ya Kati.

• "Naelewa ulikuwa ukifanya tu wajibu wako wa kulinda jamii uliponianika," sehemu ya barua hiyo ilisoma.

Mihadarati aina ya bangi
Mihadarati aina ya bangi
Image: Getty Images

Mwanamume mmoja anayedaiwa kuwa muuza bangi katika kaunti ya Kirinyaga alijisalimisha akiwa na barua aliyoandika kukiri kujihusisha katika biashara hiyo haramu na kuomba msamaha kwa asasi za kiusalama.

Katika taarifa ya Citizen, mwanamume huyo alijisalimisha mwenyewe baada ya mbunge wa Kirinyaga ya Kati Gachoki Gitari kusemekana kumwanika wiki mbili zilizopita.

Katika tukio la kushangaza kama lilivyosimuliwa na Citizen, mwanamume huyo alijiwasilisha mwenyewe kwenye ofisi ya mbunge huyo akiwa ameandamana na wachungaji wawili wa kanisa.

Pia aliwasilisha barua hiyo kwa naibu kamishna wa Kirinyaga ya Kati.

"Niwahakikishie kuwa hili halitakuwa tukio la kujirudia, naheshimu sheria pamoja na maafisa wa sheria. Naelewa ulikuwa ukifanya tu wajibu wako wa kulinda jamii uliponianika," barua hiyo iliyotiwa saini na mshukiwa na wachungaji watatu ilinukuliwa na Citizen.

"Kama naweza kuwa msaada wowote kwako na kwa jamii, tafadhali jisikie huru kuwasiliana nami. Niko tayari kutoa ushirikiano na kampeni dhidi ya dawa za kulevya."

Hili linajiri siku moja baada ya naibu rais Rigathi Gachagua kutoa tamko lake kuhusu hali mbaya ya uuzaji wa pombe haramu katika maeneo ya Mlima Kenya.

Gachagua aliomba polisi kuhakikisha visa vya pombe haramu katika eneo hilo pana vinatokomezwa.

Pia mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’wah ambaye pia ni kiongozi wa walio wengi katika bunge la kitaifa alinukuliwa akisema kuwa maeneo ya Ruaka yamegeuzwa kuwa pango la uuzaji na matumizi ya dawa kali za kulevya, na kusema kuwa eneo hilo limepiku Mombasa katika miaka 10 iliyopita kwa matumizi ya dawa kali za kulevya.