Nyeri: Jamaa amuua rafiki yake kwa kukosa kumlipa deni la shilingi 20

Jamaa huyo alimvamia mwenzake na kumchoma kisu eneo la shingo.

Muhtasari

• Miili yao ilipelekwa katika Hifadhi ya Maiti ya Hospitali ya Rufaa ya Nyeri.

Wanaume wawili walifariki katika soko la Nyeri katika mzozo wa malipo ya deni la shilingi 20.

Kulingana na taarifa ya Citizen, mwanamume mmoja mmoja alimvamia mwenzake aliyedaiwa kuwa na deni lake la shilingi 20.

Kelvin Wachira alifariki papo hapo baada ya kuchomwa kisu shingoni na mwanamume mwingine aliyetambulika kwa jina Githinji.

Githinji alijaribu kutoroka lakini umati ambao ulikuwa umefika eneo la tukio ulimpiku kwa haraka na kumshushia kipigo hadi kumuua pia.

Wawili hao baadaye walitangazwa kufariki kando kando katika Hospitali Kuu ya Mkoa wa Nyeri ambapo walikuwa wamekimbizwa kwa matibabu.

Miili yao ilipelekwa katika Hifadhi ya Maiti ya Hospitali ya Rufaa ya Nyeri.

Kwingineko, mama ambaye alirekodiwa akimuua mtoto wake kwa kumchoma kisu mara kadhaa mwilini Kitengela Jumanne alifikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa kosa la mauaji ya maksudi.

Mwanamke huyo Olivia Naserian hata hivyo hakujibu mashtaka na upande wa mashtaka uliomba azuiliwe kwa siku 10 zaidi ili kubaini iwapo ako katika hali nzuri ya kiakili kujibu mashtaka dhidi yake.

Naserian alidaiwa kumuua mtoto wake wa miaka miwili ndani ya nyumba kwa kumchoma kisu mara kadha kabla ya kunyofoa utumbo na figo yake na kubugia mdomoni.

Baadhi walihisi mwanadada huyo hakuwa katika hali sawa ya kiakili na kutaka afanyiwe uchunguzi wa akili, kwani inasemekana alipofikishwa mahakamani kwa mshangao wa wengi, aliomba kuruhusiwa kumuona mtoto wake bila kuwa na ufahamu kwamba alishamuua.